HABARI MOTO MOTO ...

Wednesday, October 31, 2012

Rushwa katika Ligi Kuu yamtoa jasho Tenga.

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga amesema kwamba vita dhidi ya rushwa katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ni ngumu na inahitaji sapoti kubwa ya wadau na wapenzi wa mchezo wenyewe ili kuifanikisha. Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, makao makuu ya TFF, Ilala mjini Dar es Salaam, Tenga alisema kwamba pamoja awali kuwepo kwa mazingira ya ushahidi wa rushwa, lakini wanashindwa kwa sababu wao wana mipaka yao. “Hili la rushwa kwa kweli ni gumu, ni gumu kwa sababu sisi tuna mipaka yetu, lazima tupate ushirikiano na vyombo husika. Lazima tupate ushirikiano wa wapenzi wenyewe wa mpira,”alisema Tenga. Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, alisema wakati mwingine inakuwa vita hiyo inakuwa ngumu zaidi anaposikia hata Waandishi wa Habari wanahusika. “Mimi sijathibitisha, lakini watu wananiambia viongozi wenyewe wanashiriki mchezo huu. Tena nasikia hadi nyinyi Waandishi wa Habari wakati mwingine mnatumiwa kupenyeza rushwa, kwa kweli inasikitisha,”alisema Tenga. Kuhusu vipimo vya dawa za kulevya katika Ligi Kuu, Tenga alisema kwamba mchakato wa zoezi hilo unaendelea na walichokifanya kwa sasa ni kuwataaribu na kuwapa muda wahusika waache taratibu. Alisema wamewapa nusu msimu watumiaji wa mihadarati katika soka ya Tanzania kujiondoa taratibu na tayari wamekwishawaambia hadi viongozi wa klabu zote, ili zoezi hilo likianza liende vizuri. “Hatutaki kuwaadhiri vijana wetu, ndiyo maana tumewaambia mapema, ili wale ambao wanavuta bangi kwa mfano, waanze taratibu kula chwingamu waache bangi, ili wakati utakapofika, hakutokuwa na mzaha,”alisema Tenga.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo, makao makuu ya shirikisho hilo, Ilala, Dar es Salaam. Kulia ni Sunday Kayuni, Mkurugenzi wa Ufundi na kushoto ni Angetile Osiah, Katibu Mkuu
Idadi ya waliofariki dunia kutokana na Kimbunga kikubwa cha Sandy huko nchini Marekani imefikia 16 ambapo zaidi ya nusu ya vifo hivyo vimetokana na watu hao kuangukiwa na miti. Vifo hivyo kwa ujumla wake vimeripotiwa katika majimbo ya New York, New Jersey, West Virginia, Connecticut, Pennsylvania na Maryland. Lakini kuna vifo vingine pia vimeripotiwa kutokana na kukatika kwa umeme na ajali ya gari katika balaa la kimbunga hicho. Kuna ripoti ya mwanamke mwingine kufariki dunia kutokana na kimbunga hicho na mwili wake kuonekana ukielea katika maeneo ya bahari,huko Toronto nchini Canada jumapili. Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha CNN Kimbunga hicho mpaka sasa kimeacha zaidi ya raia milioni 6.5 nchini Marekani pasipo nishati ya umeme katika eneo la Pwani ya Mashariki. New York ni miongoni mwa mji ulivurugwa vibaya na kimbunga hicho ambacho rekodi zinaonesha kiliambatana na mawimbi ya urefu wa meta 4 katika eneo la kusini la Manhattan. Katika eneo hilo maji yalifurika mpaka katika njia kubwa kabisa ya reli. Na soko la hisa la New York limeendelea kufungwa kwa siku ya pili mfululizo. Duru nyingine zinaeleza kwamba moto uliowaka usiku kucha umeteketeza takribani nyumba 50 katika kitongoji cha Queens. Taarifa hizo zimesambazwa na kitengo cha zimamoto kupitia ukurasa wake wa Twiter ambapo hata hivyo hakikutoa maelezo zaidi kufuatia mkasa huo. Lakini kama inavyofahamika kwamba mkasa huo umetokea baada ya kimbunga Sandy kuyakumba maeneo ya Pwani ya Mashariki ya Marekani ukiwemo mji wa New York. Hata hivyo balaa la kimbunga hicho bado halijafika kikomo ambako wasiwasi bado upo katika maeneo ya mbali ya majimbo ya Wisconsin na Ilinois. Ishara ya tahadhari imetolewa kuanzia Chicago mpaka Maine na Canada mpaka Florida. Tahadhari hiyo inaonesha kimbunga Sandy kitaendelea kuwa tatizo katika siku kadhaa zijazo na kitaambatana na mvua kali, theluji na mafuriko. Wakaazi walio katika eneo la Michigan na Ontario wametahadharishwa kuwepo kwa mawimbi makubwa. Na pia theluji zaidi kama ilivyo katika baadhi ya maeneo ya Atlantik ya kati. Hali hiyo imezorotesha kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani ambapo Rais Barack Obama na mpinzani wake Mitt Romney wanafuatilia kazi ya uokozi katika maeneo ya yalikumbwa na kimbunga hicho.

Wanaodaiwa kuchoma makanisa kuendelea kusota rumande.

WASHITAKIWA 33 wanaokabiliwa na mashitaka zaidi ya 20 likiwemo la kuchoma makanisa na kuharibu mali zenye thamani ya Sh milioni 500 wameendelea kusota rumande baada ya kukosa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Washitakiwa hao ambao jana walifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa masharti ya dhamana walishindwa kusomewa masharti hayo kwa kuwa baadhi ya mahakimu wanaosikiliza kesi hizo hawakuwepo. Washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi wa askari ambao walikuwa kwenye magari matano pamoja na gari la maji ya kuwasha. Ndugu wa washitakiwa hao waliokuwa wamesimama nje ya mahakama wakijadiliana walijikuta wakiangua kilio baada ya kuwaona ndugu zao wakipanda kwenye gari kurudishwa rumande baada ya kesi hizo kuahirishwa. Kesi hizo ziliahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi Stuart Sanga na Binge Mashambala ambapo upelelezi wa kesi hizo haujakamilika na zitatajwa tena Novemba 7 na nyingine Novemba 11 mwaka huu. Washitakiwa katika kesi hizo ni Masenga Yusuph (28), Hamad Sekondo (26), Shengo Mussa (26), Abdallah Said, Ramadhan Salum, Mashaka Iman (21), Kassim Juma (33) na wenzao 10 wanaodaiwa kuharibu mali za kanisa. Wengine ni Mwalimu Said (21), Omari Shabani, Ibrahim Msimbe, Abdallah Said, Paschal Kashiriri, Abdulkadir Haji, Ahmad Juma na Mohamed Chobe wanadaiwa kuharibu madirisha ya vioo, milango, madhabahu na mali nyingine zote zikiwa na thamani ya Sh milioni 80 mali ya kanisa la Agape Parokia ya Mbagala. Na wengine ni Hashim Ligongo (30), Abbas Said (25), Iddi Selemani (41) Yahaya Ndege (53), Daniel Ngambilile (36), Hassan Mohamed (24), Said Mkoba (22) na wenzao wanne wanadaiwa kuharibu magari mbalimbali yakiwemo ya Serikali na kufanya wizi katika baadhi ya makanisa.

FFU Arusha wawapiga mabomu wanafunzi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewapiga mabomu mamia ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kimnyaki iliyopo wilayani Arumeru walioandama kwenda katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha. Pamoja na kwenda kutoa malalamiko yao, Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo, aliagiza polisi kuwatia mbaroni wanafunzi wawili waliotoa maelezo mbele yake kuhusiana na sababu za wao kuandamana. Wanafunzi hao walifanya maandamano hayo jana wakishinikiza Mkuu wa Shule hiyo, Mariam Chamle, afukuzwe kwa tuhuma za kusababisha wanafunzi wa kidato cha nne kuwachelewesha kuingia katika chumba cha mitihani. Wanafunzi hao zaidi ya 200, walianza maandamano yao katika barabara ya Ngaramtoni, nje kidogo ya Jiji la Arusha na wakiwa njiani kuelekea katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, walikumbana na nguvu ya dola baada ya polisi kuanza kuwatawanya kwa kupiga mabomu ya machozi. Hata hivyo, pamoja na kupigwa mabomu hayo, wanafunzi hao walivumilia kwa kunawa maji usoni hadi walipofanikiwa kufika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo. MWANAFUNZI AOKOTA BOMU Mmoja wa wanafunzi hao aliokota bomu lililorushwa na polisi kabla halijalipuka akidhani kuwa ni ganda la bomu na kumuonyesha Mkuu wa Mkoa huo kama ushaidi wa jinsi walivyopigwa mabomu na polisi. Baada ya kulionyesha bomu hilo kwa Mkuu wa Mkoa, Kamanda wa Operesheni Maalum, Peter Mvulla, alimnyang’anya haraka kabla halijalipuka na kuleta madhara. Kamanda Mvulla alijitetea mbele ya Mkuu wa Mkoa na wanafunzi hao kuwa bomu hilo lilianguka kwa bahati mbaya wakati wa vurugu za kuwatuliza wasiandamane, lakini walikaidi na kuanza kuwapopa polisi kwa mawe hivyo kulazimisha kutumia nguvu ndogo kuwatuliza. Wanafunzi hao walilishutumu Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kuwapiga mabomu wakati hawakuwa na lengo baya kwa kuandamana badala ya askari wake kusikiliza kilio chao. Mesharck Lomnyaki, akizungumza kwa niaba ya wanafuzi wenzake, alidai kuwa mkuu wa shule amesababisha baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne kuchelewa kufanya mitihani yao ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa kuzuia kuingia katika chumba cha mitihani toka saa 2:00 hadi saa 4:30 alipowaruhusu kuingia. Alidai aliwazuia wanafunzi hao wasiingie kwenye chumba cha mitihani kwa madai kuwa walichelewa kuchanga michango ya shule na wengine walikuwa hawakujaza fomu za idadi ya masomo (selforms) na badala yake akawataka wazijaze siku hiyo ya mitihani huku wenzao wakiendelea kufanya mitihani. Aliongeza kuwa Oktoba 16, mwaka huu walinyimwa mwongozo wa kujibu swali la tano, lenye alama kumi kwenye somo la Kemia ambalo hawakupata kulingana na muda na kusababisha usumbufu ndani ya chumba cha mtihani na kusababisha kukata tamaa kwenye somo la Fizikia. Pia, alidai tatizo la kufanana na hilo limejitokeza kwa wanafunzi wa kidato cha pili kwenye mtihani wa Moko, na kuwa aliwafukuza wanafunzi hao kutomaliza mtihani huo kwa sababu ya kutolipa michango na kusababisha wanafunzi 46 kutofanya mtihani huo. Alisema matokeo ya kuzuia wanafunzi hao yalisababisha kushuka kwa kiwango cha ufaulu, hali iliyosababisha mwalimu huyo kutoa lugha za kashfa na kujenga woga kwa wanafunzi hao wanaotarajia kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili, utakaofanyika mwaka huu. Mwanafunzi mwingine, Ezekiel Memiri, alitaja kero nyingine wanazokumbana nazo kuwa ni pamoja na unyanyasaji wa wanafunzi na kuwa wengi hufukuzwa kwa makosa madogo madogo bila udhibitisho wa bodi ya shule. Wanafunzi hao walimuomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati kwa kumuondoa mkuu huyo wa shule kutokana na matatizo hayo ambayo yanasababisha kushuka kwa kiwango cha elimu shuleni hapo. RC AWA MBOGO Akizungumza na wanafunzi hao, Mulongo aliwasikilia huku akigeuka kuwa mbogo na kuamuru polisi kukamata wawili waliokuwa wakitoa maelezo kwa niaba ya wenzao ambao ni Meshack Lomnyaki na Daudi kwa madai kuwa walikuwa viongozi wa maandamano hayo . Alisema kumezuka tabia ya wanafunzi wa shule mbalimbali za mkoani Arusha kuandamana hata kwa makosa yasiyo na sababu hadi ofisini kwake na kwamba ameshatoa onyo kwa shule zote kuacha tabia hiyo vinginevyo atazifunga. “Shule zitakazoandamana kuanzia leo (jana) nitazifunga ili mkose kabisha masomo, maana hamtaki kusoma na leo ningefanya hivi, lakini nimeonea huruma watoto wa kike walio wengi ambao tunapigania wapate elimu. Ila hawa viongozi wenu wapelekwe ndani iwe fundisho la tabia hii,” alisema. Mulongo alitoa hadi kufika saa tisa jioni ya jana, wanafunzi hao wawe wamerejea shuleni kwao, kumsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na Afisa Elimu, vinginevyo atawafungia shule yao. “Nashangaa kupigwa mabomu, mnashangaa nini wakati mmeandamana bila kibali, mlitegemea nini mnavunja sheria na mkivunja sheria kwa kudai haki, hata haki mnayotaka hamtapata kwa sababu ya kuvunja sheria,” alisema. Hata hivyo, ilichukua muda wanafunzi hao kutawanyika kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa, wakishinikiza kuachiwa kwa wenzao wawili waliokamatwa na Polisi, hadi pale polisi walipoamua kutoweka kwa gari namba PT. 1834 na kuwaacha kwenye mataa wanafunzi hao. Baadaye wanafunzi hao waliondoka hadi makao Makuu ya polisi kusubiri wenzao waachiwe huru.

Soma habari ya kutekwa Bibi harusi na baadae kupatikana akiwa amefariki.

BI. Harusi mtarajiwa, Elizabeth Terezia (32), mkazi wa Mbezi Beach, Kinondoni jijini Dar es Salaam amebakwa, ameuawa kikatili na watu wasiojulikana wakati akitoka katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar linaloongozwa na Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima, Kwa mujibu wa bwana harusi mtarajiwa, Edefonce Sikwembe (42) ambaye ni mkazi wa Kunduchi, Dar tukio hilo la kinyama lilijiri Oktoba 10, mwaka huu majira ya usiku wakati Elizabeth akirudi nyumbani kutokea kanisani hapo. “Siku ya tukio tulikuwa katika viwanja vya kanisa la Gwajima, nilimpigia simu mwenzangu kumwambia nakwenda nyumbani kuandaa biashara ambayo ningeifanye kesho yake,” alisema Sikwembe.
“Kwa maana hiyo yeye nilimwacha kanisani. Saa 2:30 usiku nikampigia tena simu kutaka kujua alipo, akaniambia yupo njiani anaelekea nyumbani kwao. “Saa 3:00 usiku nilimpigia tena, maana ilikuwa kawaida yangu akiwa nje ya nyumbani kumfuatilia anaporudi ili nijue alipo, lakini cha kushangaza akawa hapatikani, niliamini simu yake iliishiwa chaji.
“Sikuwa na wasiwasi hata kidogo. Hata usingizi wangu usiku haukuwa wa mang’amunga’amu. Alfajiri ya siku iliyofuata nilipoamka nilimpigia simu tena nikiamini mchumba wangu Eliza alichaji simu usiku, lakini bado akawa hapatikani! “Hata hivyo, niliondoka nyumbani alfajiri hiyohiyo kwenda Buguruni ambako ndiko kuna biashara zangu. Njiani nilimfikiria sana Eliza, si kawaida yake kutopatikana hewani kwa muda wote huo. “Ilipofika saa 12 asubuhi, shemeji yangu anaitwa Lillian alinipigia simu na kuniambia Eliza tangu alipokwenda kanisani jana yake jioni hajaonekana nyumbani.
“Kuanzia hapo nilianza kupatwa na wasiwasi, tena mkubwa. Namjua Eliza, si mtu wa kwenda kulala mahali bila taarifa, hasa kwangu,”alisema bwana harusi huyo huku machozi yakimtiririka. Kabla hajaendelea, akasema kwa uchungu na kwa kifupi! “Da! Inauma sana kwa kweli.” Akaendelea: “Palepale nilifunga biashara, nikaondoka kwenda kwao ili nikapate maelezo mazuri. Lakini kabla sijafika Mbezi Beach, njiani maeneo ya Afrikana nilikutana na Lillian. “Tukaamua kwenda kanisani kwa Gwajima kwa ajili ya kuulizia. Njiani akili yangu iliwaza mengi, lakini yale mabaya sikuyapa nafasi na nilimwomba Mungu kwamba kama kuna baya lolote limemfika mpenzi wangu iwe ni filamu na si la kweli. “Tulifika, mawazo yangu yalitamani tuambiwe Eliza alilala pale kwa ajili ya huduma, lakini ikawa kinyume, tukajibiwa kuwa alipoondoka jana, hakurudi! “Kuanzia hapo nilichanganyikiwa, nilikuwa nikitembea eneo la kanisa huku na kule nikiamini nitamwona Eliza wangu, lakini bila mafanikio. “Nikaenda kuuliza kwa majirani wa maeneo yale lakini majibu yao yalikuwa hawajamuona mtu na aina hiyo. Kuna wakati nilitaka kuamini kwamba, alifichwa eneo lilelile na wafichaji waliniona ninavyohaha kumsaka mchumba wangu. “Mwishowe, mimi na Lillian tulikwenda Kituo cha Polisi Kawe na baadaye Oysterbay kwa ajili ya kuulizia na kuripoti, nako hakukuwa na taarifa za mchumba wangu. “Baada ya hapo tuliendelea kuulizia na vituo vingine vya polisi na tulifika Hospitali ya Temeke, Amana na Mwananyamala ambako pia hatukumpata Eliza. Mpaka hapo bado sikuacha kupiga simu yake na iliendelea kutopatikana.” (akatokwa machozi). Akaendelea: “Siku ya nne tangu kutoweka kwa Eliza, shemeji Lillian alinipigia simu, akaniambia niende nyumbani kwao, nikahisi Eliza ameonekana. Njiani mapigo ya moyo yalikuwa yakienda kwa kasi. “Nilipokaribia kwao, niliwaona watu wengi wakiwa katika mfereji ambao upo karibu na hapo nyumbani, nikashtuka na kusimama kwanza, kisha nikatembea tena. “Lakini tayari mwili wangu ukawa unaishiwa nguvu kwani nyuso za watu wale zilikuwa za huzuni tupu. Kusema ukweli japo ni mwanaume, nilishindwa kujizuia, nikakaa chini hasa pia baada ya kuliona ‘Difenda’ la polisi likiwa katika eneo lile.” (Sikwembe akalia tena). Alipotulia, akaendelea: “Shemeji yangu alinifuata huku akilia na kusema, ‘shemeji hatumaye Elizabeth hatunaye tena duniani.’ Sikwembe alishindwa kusimulia vizuri kutokana na kilio, lakini alisema ilionekana marehemu alitekwa na watu wasiojulikana, wakambaka na kumuua kwa kumnyonga kwa khanga kisha kutuupa mwili wake katika mfereji huo.
Alisema mwili wa marehemu ulikutwa ukielea kwenye maji machafu na umevimba huku nguo yake za ndani ikiwa pembeni yake sanjari na Biblia aliyokuwa nayo kanisani. “Elizabeth amekufa kifo cha kusikitisha sana, kinaniuma sana, maiti yake ilibidi ichukuliwe kwenye nailoni mpaka Hospitali ya Mwananyamala, lakini uongozi wa hospitali hiyo walisema chumba cha maiti kilijaa hivyo tukampeleka Muhimbili,” alisema mwanaume huyo. Marehemu alizikwa Oktoba 14, mwaka huu, Mbezi, Dar es Salaam na ilikuwa wafunge ndoa na Edefonce Desemba, mwaka huu na tayari vikao vya harusi vilishaanza kwa pande zote mbili. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.

MBEYA.

Mnamo tarehe 29-10-2012 majira ya saa10 jioni katika kijiji cha Mkola wilayani Mbozi mkoani Mbeya,askari polisi wakiwa katika dolia walimkamata Kaogoma Christopher Kashola (20,Mfipa,mkulima mkazi wa kijiji cha Mtanila akiwa na bangi debe 8 ikiwa ni sawa na kilo 25. Bangi hiyo alikuwa ameificha ndani ya nyumba yake huku mtuhumiwa huyo akiwa ni muuzaji na pia ni mvutaji wa bangi na sasa yupo mahabusu na taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea. Alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya kamishna msaidiziwa polisi Diwani Athumani alitoa wito kwa jamii kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya kwani ni hatari kwa afya zao nani kinyume na sheria.

Tuesday, October 30, 2012

Mtaa wa Mwanyanje wagoma kuchanga fedha za maendeleo

WANANCHI wa Kata ya Iganjo mkoani hapa, hawataki kuchangishwa fedha za maendeleo na viongozi wao wa Mtaa wa Mwanyanje. Sakata hilo limekuja kwa madai kwamba viongozi hao hutumia kigezo cha kuchangisha fedha za maendeleo na badala yake fedha hizo huishia ‘midomoni’ mwao. Wakizungumza katika mkutano wa mtaa huo uliofanyika hivi karibuni mtaani, hapo wananchi hao walisema wamechoshwa na michango ya kila siku isiyokuwa na tija kwa jamii. Mkutano huo uliokuwa na lengo la viongozi kuwaeleza wananchi juu ya mchango wa ujenzi wa chumba cha maabara katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Iganjo uligomewa baada ya wananchi kuhoji matumizi ya baadhi ya fedha zao walizochanga awali. “Mwenyekiti hebu tuelezeni, tulichanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mtaani, lakini hadi sasa fedha hizo hatujui zimekwenda wapi,” alisema Oswadi Maenga. Maenga alisema wananchi wa mtaa huo wanahitaji maendeleo na wala si siasa kama wanavyofanya viongozi hao. Naye mwalimu mmoja (jina tunalo) aliutuhumu uongozi huo kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Hasenshelo inayotumiwa na mitaa mitatu ya Mwanyenje, Ishinga na Mtakuja. Alisema pamoja na wananchi kujitahidi kuchangia jengo hilo hadi kufikia usawa wa linta, matofali yote yameibwa na kusababisha jengo hilo kurudi katika hatua ya awali. Akijibu hoja za wananchi hao, Mwenyekiti wa mtaa huo, Anthony Mwalyambi (CCM) alikiri kuwepo kwa upungufu katika safu yake ya uongozi na kuahidi kuyafanyia kazi na kuzitafuta fedha zote zilizowahi kuchangishwa kwa kuandaa mapato na matumizi ya fedha hizo. Katika hatua nyingine aliyekuwa mjumbe wa serikali ya mtaa huo na Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu David Edward (CCM) alijiuzulu na kusema kuwa amefanya hivyo kutokana na mwenyekiti wake kuendesha mtaa kama nyumbani kwake.

Monday, October 29, 2012

Uamuzi pingamizi kesi ya ubunge wa Lema Novemba 29.

UAMUZI wa pingamizi zilizowekwa na mawakili wa pande zote mbili katika kesi ya uchaguzi, Jimbo la Arusha Mjini dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa Chadema, Godbless Lema utatolewa Novemba 29, mwaka huu. Awali, upande wa wajibu rufani katika kesi iliyomng’oa madarakani Lema, Alute Mughwai ambaye ni Wakili wa wanachama watatu wa CCM, aliiomba Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa hiyo iliyowasilishwa kwao kwa kuwa ni batili na ina makosa mengi ya kisheria. Wakili Mughwai alisema mwishoni mwa wiki mjini Arusha kwamba wamepokea hati ya Mahakama Kuu ikiwajulisha juu ya hatua hiyo ya uamuzi huo kusikilizwa jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, jana Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa Kanda ya Dar es Salaam, Zahra Maruma alisema uamuzi wa pingamizi zilizowekwa na pande zote mbili katika rufaa ya Lema, haipo kwenye orodha ya kesi zinazosikilizwa Novemba mwaka huu. Hata hivyo, alisema uamuzi huo unatarajia kutolewa kabla ya Novemba 29, mwaka huu na pande zote mbili zitapewa tarehe ya kusomwa kwa uamuzi wa pingamizi hizo. Katika hoja zake, Mughwai aliwaeleza majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mkuu Othmani Chande kuwa kesi hiyo ni batili kwa kuwa imekosa vitu muhimu vya kisheria ikiwamo tarehe ya rufaa hiyo kuandaliwa, kulalamikia kipengele ambacho hakijamtoa Lema madarakani pamoja na kutokuwa na muhuri wa Mahakama Kuu iliyoidhinisha rufaa hiyo. Mughwai alidai katika nakala ya hati ya kukazia hukumu iliyowasilishwa mahakamani hapo, haina tarehe ya kuandaliwa kwake hali inayotia wasiwasi iwapo itakuwa imeandaliwa ndani ya kipindi kinachotakiwa kisheria cha siku 60 tangu kutolewa kwa hukumu au la, Aidha, haikuwa na muhuri wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuthibitisha kuwa ni kweli imetolewa na mahakama hiyo kwa kuwa nakala hiyo ilikuwa na saini tu ya Jaji Gabriel Rwakibarila ambayo haithibitishi uhalali wake. Wakili wa waomba rufaa, Method Kimomogoro alikiri kuwa ni kweli nakala hiyo ina upungufu na ni makosa ya kibinadamu ambayo hayana athari katika kesi ya msingi, hivyo kuwaomba majaji kuyatupilia mbali. Aidha, Wakili wa Serikali, Timon Vitalis alidai suala hilo la upungufu, lawama hazipaswi kuelekezwa kwa waomba rufani wala mawakili, bali zinapaswa kuelekezwa kwa mahakama iliyoandaa hati hiyo.

Nassari hakufyatua risasi kwenye uchaguzi mdogo wa Daraja Mbili – Polisi

POLISI mkoani Arusha imesema kwamba aliyefyatua risasi katika vurugu kwenye Uchaguzi Mdogo wa udiwani Kata ya Daraja Mbili ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), God Mwalusamba na si Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema). Aidha, watu 10 ambao ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuleta vurugu katika uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili. Akithibitisha kufikishwa mahakamani kwa wafuasi hao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema ni baada ya uchunguzi kukamilika. Sabas alisema wafuasi hao walileta vurugu kubwa zilizotokea katika kata hiyo huku wakiwa na silaha za jadi ambazo ziliwajeruhi baadhi ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi. Alisema vurugu hizo zilimfanya Mwalusamba kufyatua risasi nne hewani ili kuwaokoa baadhi ya vijana wa CCM waliozingirwa na wafuasi wa Chadema na kama isingefanyika hivyo, hali ilikuwa mbaya. “Unajua bila Mwalusamba kufyatua risasi nne hewani, hali ilikuwa mbaya sana kwani vijana wengi wangepata madhara na hata vifo vingetokea, lakini hatuombi hivyo,” alisema Kamanda Sabas. Kamanda huyo alisema katika vurugu zote hizo, walikuwapo Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Nassari, lakini mbunge huyo wa Arumeru Mashariki hakupiga risasi yoyote. Alisema pamoja na kwamba katika vurugu hizo huwezi kujua nani kapiga risasi hewani na nani hakupiga, lakini taarifa za kipolisi zimegundua kuwa Mwalusamba ndiye aliyepiga risasi hewani kuwaokoa vijana wa UVCCM na sio Nassari. Kwa upande wake, Nassari alisisitiza jana kwamba licha ya kuwapo kwenye eneo hilo mapema juzi asubuhi, hakufyatua risasi, na kwamba taarifa zilizoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari ilikuwa na nia ya kumchafua kisiasa, lakini kwa imani yake anaamini Mungu atampitisha katika majaribu na vita hiyo. Nassari aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ni kweli alipita eneo la Daraja Mbili mapema juzi asubuhi kuwashusha mawakala wa uchaguzi kisha yeye alikwenda Bang’ata wilayani Arumeru kusimamia uchaguzi kama wakala mkuu kupitia chama chake hadi usiku wa manane.

Vibaka walitaka kuniuwa mbele ya kituo cha Polisi Salender.

MBUNGE wa Iringa Mjini, (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa, ameeleza namna alivyovamiwa, kupigwa na kuporwa na vibaka maeneo ya Daraja la Salenda, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akisimulia mkasa huo jana, Mchungaji Msigwa alisema, alikabwa na vibaka juzi, saa moja usiku wakati akitokea katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Siku hiyo Kamati yetu ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, tulikuwa tumekwenda kutembelea Msitu wa Ruvu Kusini na wakati narudi nilipitia ile Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
“Nilipofika maeneo ya Daraja la Salenda Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ghafla gari yangu ilipata hitilafu katika upande wa tairi, ndipo nikashuka pamoja na dereva wangu ili kukagua.
“Kabla ya kushuka, nilimwambia dereva wangu anayeitwa Baraka, apaki pembeni kidogo ili asisababishe foleni. Tulipolikagua gari, tukakuta kuna kasoro zilizosababisha tairi zisiweze kuzunguka vizuri.
“Dereva wangu alichukua jeki na kuanza kutengeneza gari, wakati huo mimi nikawa nazungumza na mtu kwenye simu yangu, pembeni ya ukuta wa daraja. Ghafla mbele yangu wakatokea vijana kama nane hivi, wakawa wananisogelea, mimi nikaamini wale labda wamekuja kunisaidia kumbe sio.
“Waliponikaribia, nikawauliza wanataka nini, wakaniambia kaa kimya, kwa kuwa mimi ni mbishi, nikaendelea kuzungumza na simu, lakini mmoja wao akaanza kuninyang’anya ile simu nikawa naing’ang’ania, kwa sababu najua ina namba nyingi za watu.
“Nilipozidi kuonyesha ubishi walizidi kunikaba, wakati huo baadhi yao waliendelea kumminya dereva wangu ambaye tayari alikuwa kule chini ya gari akilitengeneza.
“Lakini mimi nikapambana na wawili niliokuwa nao nikawa nakaribia kuwashinda, hata hivyo wakaongezeka tena, ndipo wakafanikiwa kunidhibiti na kuninyang’anya simu yangu na nyingine zilikuwa kwenye gari, wakachukua pia na fedha taslimu Sh 400,000 na baadhi ya vitu vidogo vidogo vilivyokuwa kwenye gari, isipokuwa Ipad hawakufanikiwa kuiona kwa sababu ilikuwa kwenye kioo cha mbele cha gari.
“Kusema kweli walinipiga kisawasawa, wakaniumiza mguu kidogo na jicho, wakaniharibia na meno yangu mawili ya bandia.
“Wakati wananikaba, wengine walimkamata dereva wangu na kumtupa baharini, lakini nashukuru hakudhurika. Baadaye tukapata msaada kwa askari polisi waliofika eneo la tukio, ingawa walichelewa kufika.
“Hata hivyo, sasa hali yangu inaendelea vizuri kwa sababu hapo awali nilikuwa na tatizo la mguu, ambao mwezi uliopita nilikwenda Ujerumani nikaanguka na kufanyiwa uchunguzi, lakini niliporudi nchini Oktoba tisa, nilifanyiwa upasuaji na sasa naendelea vizuri kwa sababu nategemea kutoa hili hogo kesho,” alisema Mchungaji Msigwa.
Akizungumzia eneo hilo jinsi lilivyo, alisema limekuwa na historia ya watu kukabwa na kuibiwa fedha na vitu mbalimbali.
“Kwanza ni aibu sana kwa sababu ni eneo ambalo lipo karibu na Kituo cha Polisi, lakini ukiwauliza askari wanadai eti wakitaka kuwakamata hao vibaka huwa wanakimbilia baharini.
“Wapo pia wabunge mbalimbali nimesikia walishawahi kukabwa hapo na kuibiwa Sh milioni moja, ingawa hawakutaka kusema, mimi ni msema kweli nimesema kwamba walinikaba.
“Vivyo hivyo, nilishawahi kusikia huyu Kigogo wa JWTZ anayeitwa Shimbo, naye alishawahi kukabwa baada ya kufika eneo hilo baada ya kushuka kwenye gari na kuanza kujisadia haja ndogo,” alisema.
Kwa mujibu wa habari iliyochapishwa na gazeti moja linalochapishwa kila siku toleo la jana (siyo MTANZANIA), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Komba, alisema vibaka wawili wameshakamatwa na leo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Vikao vya Bunge kuanza kesho mjini Dodoma.

MKUTANO wa Tisa wa Bunge la Muungano unatarajia kuanza kesho Mjini Dodoma, huku ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge iliyoundwa kuchunguza tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge ikisubiriwa kwa hamu kubwa.
Tume hiyo inayoongozwa na Hassan Ngwilizi iliundwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo zilizoibuka katika mkutano wa Bunge uliopita. Tuhuma hizo ndizo zilizomfanya Spika kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo, Agosti mwaka huu, Makinda aliunda tume ya wabunge watano kuchunguza tuhuma hizo.
Ripoti hiyo inatarajiwa kuwa mtihani mkubwa kwa Spika Makinda hasa ikizingatiwa kwamba ndiye mwenye mamlaka ya kuwasilisha ripoti hiyo bungeni hasa kutokana na kuibuka kwa maneno ya chinichini kwamba kumekuwa na jitihada za kuwasafisha wabunge hasa wa chama tawala.
Hivi karibuni, Naibu Spika, Job Ndugai alikaririwa akisema kuwa mamlaka ya namna ya kuiwasilisha ripoti hiyo yako mikononi mwa Spika Makinda.
“Kwa kawaida na kanuni zetu ni kwamba Spika anaweza kuamua kama ripoti hiyo ijadiliwe au iwasilishwe kwa njia ipi, wala hawezi kuingiliwa,” alisema Ndugai.
Mbali na ripoti hiyo, Mkutano huo wa Bunge ambao utadumu kwa wiki mbili, pia unatarajiwa kupokea hoja binafsi kutoka kwa Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jaffo kuhusu mifuko ya jamii.
Jaffo aliibua hoja hiyo katika mkutano uliopita akitaka itungwe sheria ya kufanya marekebisho ili kipengele kinachomtaka mwanachama wa mfuko kupewa mafao yake pindi anapofikisha umri wa miaka 55 kiondolewe.
Wakati huohuo, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi walianza kuwasili Dodoma jana tayari kwa mkutano wa uchaguzi unaotarajia kuanza kesho.
Awali, mkutano huo uliokuwa ufanyike Oktoba 27 hadi 28, lakini ulisogezwa mbele ili kupisha waumini wa dini ya Kiislamu kuungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Idd El Haj.
Katika uchaguzi huo nafasi ya mwenyekiti inagombewa na Abdallah Bulembo na John Barongo na Martha Mlata.
Tayari Jumuiya nyingine za CCM za Umoja wa Vijana (UVCCM) na UWT zimeshafanya uchaguzi wa viongozi wake wa juu wa kuziongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
Katika chaguzi hizo, UVCCM ilimchagua Khamis Sadifa Juma kuwa mwenyekiti wake mpya wakati Sofia Simba alichaguliwa tena kuongoza UWT.

Usafiri wa Treni wazinduliwa rasmi Jijini Dar Es Salaam.

Na Joachim Mushi, Thehabari.com
USAFIRI wa kutumia treni jijini Dar es Salaam kutokea eneo la Ubungo Maziwa kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Stesheni ya Treni) umeanza leo. Treni ya kwanza imeondoka Ubungo majira ya saa 12:00 asubuhi kuelekea katikati ya jiji, ambapo kwa mujibu wa maofisa wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) imetumia wastani wa dakika 30 kufika katikati ya jiji.
Treni ilioanza kazi leo iliyokuwa na injini mbili (vichwa vya traini) moja ikiwa imefungwa nyuma na nyingine mbele huku ikiwa na mabehewa sita, yaani matano ya abiria wa kawaida (watu wazima) na moja likiwa ni maalumu kwa ajili ya kubeba wanafunzi. Abiria mmoja ni sh. 400 kwa tripu huku wanafunzi wakitakiwa kulipa sh. 100 kwa kila mmoja.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ndiye aliyezindua usafiri wa leo ambao ni wamajaribio, akiwa pamoja na viongozi waandamizi kutoka TRC, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja na Polisi Kitengo cha Reli. Treni hiyo pia imezinduliwa pamoja na treni ya TAZARA ambayo itafanya kazi kama ya Ubungo, lakini yenyewe ikianzia eneo la TAZARA kuelekea Mwakanga.
Akizungumza mara baada ya ufunguzi huo Waziri Mwakyembe alisema atahakikisha treni hiyo inaendelea kufanya kazi ili kuwasaidia kiusafiri wananchi wa Dar es Salaam ambao wamekuwa wakisumbuliwa na kero ya usafiri hasa kwa foleni, ambapo utumia muda mrefu njiani kuingia na kutoka jijini.
Alisema jumla ya mabehewa ya treni 14 pamoja na injini mbili zimekarabatiwa na mafundi wazalendo nchini, ambayo ndiyo yatakayokuwa yakifanya kazi ya kusafirisha abiria kuingia na kutoka jijini kila asubuhi na jioni. Alisema kwa sasa inafanya treni moja kwa majaribio lakini baada ya uzinduzi mkubwa zitafanya kazi treni mbili, na zitakuwa zikipishana njiani moja ikirudi na nyingine ikienda.
Akifafanua zaidi alisema kitendo cha mafundi wazalendo kufanya ukarabati kwa mabehewa na injini kimeokoa kiasi kikubwa cha fedha za umma kwani ukarabati wote umetumia sh. bilioni 2.1 tu, ilhali kama Serikali ingelazimika kukodi injini gharama ingekuwa kubwa zaidi kwani bei ya kukodi injini moja ya treni ni sh. milioni moja kwa siku.
Hata hivyoDk. Mwakyembe amewataka Watanzania hasa abiria kuwa wavumilivu kwa upungufu utakaojitokeza kwa safari za mwanzo kwani bado wanaendelea kufanya marekebisho kadhaa, lakini baada ya muda mambo yatakaa sawa. Mwandishi wa habari hizi alikuwa ni mmoja wa wasafiri walioizindua treni hiyo leo.
Awali akizungumza mmoja wa viongozi waandamizi wa TRC, alisema treni hiyo itafanya kazi kila siku isipokuwa kwa siku za jumapili na siku kuu na itaanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa sita mchana na kupumzika hadi saa 9:00 za jioni, itakapoendelea tena na safari zake hadi majira ya saa nne usiku.
Uchunguzi uliofanywa na muandishi wa habari hizi umebaini kuwa behewa moja la treni linauwezo wa kuchukua abiria 66 wakiwa wamekaa, lina milango minne, feni, taa, muziki/redio, pamoja na mikanda maalumu ya kujishikia kwa abiria ambao watakuwa wamesimama.
Aidha mabehewa yote yana madirisha ya kutosha kuingiza na kutoa hewa ya kutosha. Treni ilioanza kazi leo, ikitokea Ubungo ilikuwa ikisimama vituo vya eneo la Mwananchi (relini), Tabata Relini, Buguruni Miamani, Tazara, Kariakoo Gerezani (Kamata), na mwisho Kituo Kikuu cha Treni kilichopo jirani na Kituo cha Polisi Kati (Katikati ya Jiji)

Nassari hakufyatua risasi kwenye uchaguzi mdogo wa Daraja Mbili – Polisi

POLISI mkoani Arusha imesema kwamba aliyefyatua risasi katika vurugu kwenye Uchaguzi Mdogo wa udiwani Kata ya Daraja Mbili ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), God Mwalusamba na si Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema).
Aidha, watu 10 ambao ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuleta vurugu katika uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili.
Akithibitisha kufikishwa mahakamani kwa wafuasi hao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema ni baada ya uchunguzi kukamilika.
Sabas alisema wafuasi hao walileta vurugu kubwa zilizotokea katika kata hiyo huku wakiwa na silaha za jadi ambazo ziliwajeruhi baadhi ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi.
Alisema vurugu hizo zilimfanya Mwalusamba kufyatua risasi nne hewani ili kuwaokoa baadhi ya vijana wa CCM waliozingirwa na wafuasi wa Chadema na kama isingefanyika hivyo, hali ilikuwa mbaya.
“Unajua bila Mwalusamba kufyatua risasi nne hewani, hali ilikuwa mbaya sana kwani vijana wengi wangepata madhara na hata vifo vingetokea, lakini hatuombi hivyo,” alisema Kamanda Sabas.
Kamanda huyo alisema katika vurugu zote hizo, walikuwapo Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Nassari, lakini mbunge huyo wa Arumeru Mashariki hakupiga risasi yoyote.
Alisema pamoja na kwamba katika vurugu hizo huwezi kujua nani kapiga risasi hewani na nani hakupiga, lakini taarifa za kipolisi zimegundua kuwa Mwalusamba ndiye aliyepiga risasi hewani kuwaokoa vijana wa UVCCM na sio Nassari.
Kwa upande wake, Nassari alisisitiza jana kwamba licha ya kuwapo kwenye eneo hilo mapema juzi asubuhi, hakufyatua risasi, na kwamba taarifa zilizoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari ilikuwa na nia ya kumchafua kisiasa, lakini kwa imani yake anaamini Mungu atampitisha katika majaribu na vita hiyo.
Nassari aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ni kweli alipita eneo la Daraja Mbili mapema juzi asubuhi kuwashusha mawakala wa uchaguzi kisha yeye alikwenda Bang’ata wilayani Arumeru kusimamia uchaguzi kama wakala mkuu kupitia chama chake hadi usiku wa manane.