HABARI MOTO MOTO ...
Tuesday, October 30, 2012
Mtaa wa Mwanyanje wagoma kuchanga fedha za maendeleo
WANANCHI wa Kata ya Iganjo mkoani hapa, hawataki kuchangishwa fedha za maendeleo na viongozi wao wa Mtaa wa Mwanyanje.
Sakata hilo limekuja kwa madai kwamba viongozi hao hutumia kigezo cha kuchangisha fedha za maendeleo na badala yake fedha hizo huishia ‘midomoni’ mwao.
Wakizungumza katika mkutano wa mtaa huo uliofanyika hivi karibuni mtaani, hapo wananchi hao walisema wamechoshwa na michango ya kila siku isiyokuwa na tija kwa jamii.
Mkutano huo uliokuwa na lengo la viongozi kuwaeleza wananchi juu ya mchango wa ujenzi wa chumba cha maabara katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Iganjo uligomewa baada ya wananchi kuhoji matumizi ya baadhi ya fedha zao walizochanga awali.
“Mwenyekiti hebu tuelezeni, tulichanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mtaani, lakini hadi sasa fedha hizo hatujui zimekwenda wapi,” alisema Oswadi Maenga.
Maenga alisema wananchi wa mtaa huo wanahitaji maendeleo na wala si siasa kama wanavyofanya viongozi hao.
Naye mwalimu mmoja (jina tunalo) aliutuhumu uongozi huo kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Hasenshelo inayotumiwa na mitaa mitatu ya Mwanyenje, Ishinga na Mtakuja.
Alisema pamoja na wananchi kujitahidi kuchangia jengo hilo hadi kufikia usawa wa linta, matofali yote yameibwa na kusababisha jengo hilo kurudi katika hatua ya awali.
Akijibu hoja za wananchi hao, Mwenyekiti wa mtaa huo, Anthony Mwalyambi (CCM) alikiri kuwepo kwa upungufu katika safu yake ya uongozi na kuahidi kuyafanyia kazi na kuzitafuta fedha zote zilizowahi kuchangishwa kwa kuandaa mapato na matumizi ya fedha hizo.
Katika hatua nyingine aliyekuwa mjumbe wa serikali ya mtaa huo na Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu David Edward (CCM) alijiuzulu na kusema kuwa amefanya hivyo kutokana na mwenyekiti wake kuendesha mtaa kama nyumbani kwake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment