POLISI mkoani Arusha imesema kwamba aliyefyatua risasi katika vurugu
kwenye Uchaguzi Mdogo wa udiwani Kata ya Daraja Mbili ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), God Mwalusamba na si Mbunge wa
Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema).
Aidha, watu 10 ambao ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuleta vurugu katika
uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili.
Akithibitisha kufikishwa mahakamani kwa wafuasi hao, Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema ni baada ya uchunguzi
kukamilika.
Sabas alisema wafuasi hao walileta vurugu kubwa zilizotokea katika
kata hiyo huku wakiwa na silaha za jadi ambazo ziliwajeruhi baadhi ya
vijana wa Chama Cha Mapinduzi.
Alisema vurugu hizo zilimfanya Mwalusamba kufyatua risasi nne hewani
ili kuwaokoa baadhi ya vijana wa CCM waliozingirwa na wafuasi wa Chadema
na kama isingefanyika hivyo, hali ilikuwa mbaya.
“Unajua bila Mwalusamba kufyatua risasi nne hewani, hali ilikuwa
mbaya sana kwani vijana wengi wangepata madhara na hata vifo vingetokea,
lakini hatuombi hivyo,” alisema Kamanda Sabas.
Kamanda huyo alisema katika vurugu zote hizo, walikuwapo Mbunge wa
zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Nassari, lakini mbunge huyo wa
Arumeru Mashariki hakupiga risasi yoyote.
Alisema pamoja na kwamba katika vurugu hizo huwezi kujua nani kapiga
risasi hewani na nani hakupiga, lakini taarifa za kipolisi zimegundua
kuwa Mwalusamba ndiye aliyepiga risasi hewani kuwaokoa vijana wa UVCCM
na sio Nassari.
Kwa upande wake, Nassari alisisitiza jana kwamba licha ya kuwapo
kwenye eneo hilo mapema juzi asubuhi, hakufyatua risasi, na kwamba
taarifa zilizoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari ilikuwa na nia ya
kumchafua kisiasa, lakini kwa imani yake anaamini Mungu atampitisha
katika majaribu na vita hiyo.
Nassari aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ni kweli alipita
eneo la Daraja Mbili mapema juzi asubuhi kuwashusha mawakala wa uchaguzi
kisha yeye alikwenda Bang’ata wilayani Arumeru kusimamia uchaguzi kama
wakala mkuu kupitia chama chake hadi usiku wa manane.
No comments:
Post a Comment