HABARI MOTO MOTO ...
Monday, October 29, 2012
Uamuzi pingamizi kesi ya ubunge wa Lema Novemba 29.
UAMUZI wa pingamizi zilizowekwa na mawakili wa pande zote mbili katika kesi ya uchaguzi, Jimbo la Arusha Mjini dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa Chadema, Godbless Lema utatolewa Novemba 29, mwaka huu.
Awali, upande wa wajibu rufani katika kesi iliyomng’oa madarakani Lema, Alute Mughwai ambaye ni Wakili wa wanachama watatu wa CCM, aliiomba Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa hiyo iliyowasilishwa kwao kwa kuwa ni batili na ina makosa mengi ya kisheria.
Wakili Mughwai alisema mwishoni mwa wiki mjini Arusha kwamba wamepokea hati ya Mahakama Kuu ikiwajulisha juu ya hatua hiyo ya uamuzi huo kusikilizwa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, jana Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa Kanda ya Dar es Salaam, Zahra Maruma alisema uamuzi wa pingamizi zilizowekwa na pande zote mbili katika rufaa ya Lema, haipo kwenye orodha ya kesi zinazosikilizwa Novemba mwaka huu.
Hata hivyo, alisema uamuzi huo unatarajia kutolewa kabla ya Novemba 29, mwaka huu na pande zote mbili zitapewa tarehe ya kusomwa kwa uamuzi wa pingamizi hizo.
Katika hoja zake, Mughwai aliwaeleza majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mkuu Othmani Chande kuwa kesi hiyo ni batili kwa kuwa imekosa vitu muhimu vya kisheria ikiwamo tarehe ya rufaa hiyo kuandaliwa, kulalamikia kipengele ambacho hakijamtoa Lema madarakani pamoja na kutokuwa na muhuri wa Mahakama Kuu iliyoidhinisha rufaa hiyo.
Mughwai alidai katika nakala ya hati ya kukazia hukumu iliyowasilishwa mahakamani hapo, haina tarehe ya kuandaliwa kwake hali inayotia wasiwasi iwapo itakuwa imeandaliwa ndani ya kipindi kinachotakiwa kisheria cha siku 60 tangu kutolewa kwa hukumu au la, Aidha, haikuwa na muhuri wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuthibitisha kuwa ni kweli imetolewa na mahakama hiyo kwa kuwa nakala hiyo ilikuwa na saini tu ya Jaji Gabriel Rwakibarila ambayo haithibitishi uhalali wake.
Wakili wa waomba rufaa, Method Kimomogoro alikiri kuwa ni kweli nakala hiyo ina upungufu na ni makosa ya kibinadamu ambayo hayana athari katika kesi ya msingi, hivyo kuwaomba majaji kuyatupilia mbali.
Aidha, Wakili wa Serikali, Timon Vitalis alidai suala hilo la upungufu, lawama hazipaswi kuelekezwa kwa waomba rufani wala mawakili, bali zinapaswa kuelekezwa kwa mahakama iliyoandaa hati hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment