Tume hiyo inayoongozwa na Hassan Ngwilizi iliundwa na Spika wa Bunge,
Anne Makinda kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo zilizoibuka katika
mkutano wa Bunge uliopita. Tuhuma hizo ndizo zilizomfanya Spika kuivunja
Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo, Agosti mwaka huu, Makinda aliunda tume ya wabunge watano kuchunguza tuhuma hizo.
Ripoti hiyo inatarajiwa kuwa mtihani mkubwa kwa Spika Makinda hasa
ikizingatiwa kwamba ndiye mwenye mamlaka ya kuwasilisha ripoti hiyo
bungeni hasa kutokana na kuibuka kwa maneno ya chinichini kwamba
kumekuwa na jitihada za kuwasafisha wabunge hasa wa chama tawala.
Hivi karibuni, Naibu Spika, Job Ndugai alikaririwa akisema kuwa
mamlaka ya namna ya kuiwasilisha ripoti hiyo yako mikononi mwa Spika
Makinda.
“Kwa kawaida na kanuni zetu ni kwamba Spika anaweza kuamua kama
ripoti hiyo ijadiliwe au iwasilishwe kwa njia ipi, wala hawezi
kuingiliwa,” alisema Ndugai.
Mbali na ripoti hiyo, Mkutano huo wa Bunge ambao utadumu kwa wiki
mbili, pia unatarajiwa kupokea hoja binafsi kutoka kwa Mbunge wa
Kisarawe (CCM), Suleiman Jaffo kuhusu mifuko ya jamii.
Jaffo aliibua hoja hiyo katika mkutano uliopita akitaka itungwe
sheria ya kufanya marekebisho ili kipengele kinachomtaka mwanachama wa
mfuko kupewa mafao yake pindi anapofikisha umri wa miaka 55 kiondolewe.
Wakati huohuo, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi
wa Chama Cha Mapinduzi walianza kuwasili Dodoma jana tayari kwa mkutano
wa uchaguzi unaotarajia kuanza kesho.
Awali, mkutano huo uliokuwa ufanyike Oktoba 27 hadi 28, lakini
ulisogezwa mbele ili kupisha waumini wa dini ya Kiislamu kuungana na
wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Idd El Haj.
Katika uchaguzi huo nafasi ya mwenyekiti inagombewa na Abdallah Bulembo na John Barongo na Martha Mlata.
Tayari Jumuiya nyingine za CCM za Umoja wa Vijana (UVCCM) na UWT
zimeshafanya uchaguzi wa viongozi wake wa juu wa kuziongoza kwa kipindi
cha miaka mitano.Katika chaguzi hizo, UVCCM ilimchagua Khamis Sadifa Juma kuwa mwenyekiti wake mpya wakati Sofia Simba alichaguliwa tena kuongoza UWT.
No comments:
Post a Comment