HABARI MOTO MOTO ...

Wednesday, October 31, 2012

Wanaodaiwa kuchoma makanisa kuendelea kusota rumande.

WASHITAKIWA 33 wanaokabiliwa na mashitaka zaidi ya 20 likiwemo la kuchoma makanisa na kuharibu mali zenye thamani ya Sh milioni 500 wameendelea kusota rumande baada ya kukosa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Washitakiwa hao ambao jana walifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa masharti ya dhamana walishindwa kusomewa masharti hayo kwa kuwa baadhi ya mahakimu wanaosikiliza kesi hizo hawakuwepo. Washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi wa askari ambao walikuwa kwenye magari matano pamoja na gari la maji ya kuwasha. Ndugu wa washitakiwa hao waliokuwa wamesimama nje ya mahakama wakijadiliana walijikuta wakiangua kilio baada ya kuwaona ndugu zao wakipanda kwenye gari kurudishwa rumande baada ya kesi hizo kuahirishwa. Kesi hizo ziliahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi Stuart Sanga na Binge Mashambala ambapo upelelezi wa kesi hizo haujakamilika na zitatajwa tena Novemba 7 na nyingine Novemba 11 mwaka huu. Washitakiwa katika kesi hizo ni Masenga Yusuph (28), Hamad Sekondo (26), Shengo Mussa (26), Abdallah Said, Ramadhan Salum, Mashaka Iman (21), Kassim Juma (33) na wenzao 10 wanaodaiwa kuharibu mali za kanisa. Wengine ni Mwalimu Said (21), Omari Shabani, Ibrahim Msimbe, Abdallah Said, Paschal Kashiriri, Abdulkadir Haji, Ahmad Juma na Mohamed Chobe wanadaiwa kuharibu madirisha ya vioo, milango, madhabahu na mali nyingine zote zikiwa na thamani ya Sh milioni 80 mali ya kanisa la Agape Parokia ya Mbagala. Na wengine ni Hashim Ligongo (30), Abbas Said (25), Iddi Selemani (41) Yahaya Ndege (53), Daniel Ngambilile (36), Hassan Mohamed (24), Said Mkoba (22) na wenzao wanne wanadaiwa kuharibu magari mbalimbali yakiwemo ya Serikali na kufanya wizi katika baadhi ya makanisa.

No comments:

Post a Comment