HABARI MOTO MOTO ...

Wednesday, November 28, 2012

Magufuli aja juu kwa nesi kunyofoa drip za watoto 7





Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameingilia kati sakata la muuguzi afya (nesi) wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita la kuwanyofolea chupa za maji ya dawa (drip) watoto saba waliolazwa hospitalini hapo.
Kutokana na tukio hilo ambalo lingeweza kusababisha vifo, Waziri Magufuli alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) wa Chato kumkamata na kumfikisha mahakamani nesi huyo (jina tunalihifadhi) kwa kitendo hicho.
Inadaiwa kuwa nesi huyo alifikia maamuzi ya kuwaadhibu watoto kwa kuwakatia dawa baada wazazi wao kukataa kufanya usafi kwenye vyoo vya hospitali hiyo.
Tukio hilo ambalo limetokea jana majira ya asubuhi liliwalazimisha wazazi wa watoto hao kufanya mawasiliano na Mganga Mkuu wa hospitali hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya ndugu wa watoto hao walipiga simu kwa Katibu wa Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi aliyewasili hopitalini hapo akifuatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.
Akizungumza na wagonjwa, madaktari na wauguzi (manesi) na wahudumu wa afya, Dk. Magufuli alisema kitendo kilichofanywa na nesi huyo hakistahili kufumbiwa macho kwa kuwa kililenga kupoteza uhai wa wagonjwa waliokuwa wanaendelea kutumia dawa kutokana na maelekezo waliyopewa na madaktari.
Alisema kutokana na malalamiko mengi ya wagonjwa kuhusiana na huduma za afya zinazotolewa hospitalini hapo, kuna haja ya kutafuta mwarobaini wa kutibu vitendo vya ukiukwaji wa sheria vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Idara ya Afya ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea.
Kufuatia hali hiyo, Magufuli alimwagiza OCD wa Chato, Leonard Nyaoga, kuhakikisha Jeshi lake linamsaka na kumfikisha mahakamani nesi huyo kwa tuhuma za kutaka kusababisha vifo vya watu saba kinyume cha sheria.
Vilevile amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Shaban Ntarambe, kumsimamisha kazi mara moja wakati taratibu za kisheria zikiwa zinaendelea na kwamba hatakiwi kuonekana akitoa huduma kwenye hospitali hiyo kwa kuwa kitendo chake kimethibitisha kuwa hana sifa za kuwa muuguzi.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, ambaye aliongozana na Waziri Magufuli, alisema serikali inalishughulikia tukio hilo mpaka hapo sheria itakapochukua mkondo wake kwa kuwa kitendo kilichofanywa na muuguzi huyo siyo cha kiuungwana.
Mpongolo aliwataka wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kupata matibabu kutoa ushirikiano kwa viongozi wa hospitali yanapotokea matukio ambayo yanaweza kuhatarisha maisha kutokana na utendaji kazi mbovu wa baadhi ya watumishi.
Pia, aliahidi kuunda kamati maalum itakayochunguza huduma za afya zinazotolewa katika hospitali hiyo kufuatia malalamiko mengi ya wananchi.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Pius Buchukundi, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba ofisi yake imekwisha kuchukua hatua za kuhakikisha mtumishi huyo anawajibishwa kulingana na kosa alilotenda.
Dk. Buchukundi alisema kitendo cha watoto saba kuondolewa maji yenye dawa hakikufanywa kwa maelekezo ya uongozi wa hospitali hiyo bali ni maamuzi binafsi ya mtumishi huyo kwa matakwa yake binafsi.
Aliwahakikishia wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali hiyo kuwa tukio kama hilo halitajitokeza tena.
Aliwataja watoto ambao walinyofolewa drip kuwa ni Edward Robert (4), mkazi wa kijiji cha Nyamirembe; Kashinje Lukanya (12), mkazi wa Busaka; Iren Nasib (3), mkazi wa Bwanga; Naomi Tumain (5), mkazi wa Kachwamba; Yunis William (3), mkazi wa Kasala; Asteria Siajali (2), mkazi wa Kahumo na Alphonce Makolobelo.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, Ester Misungwi, Sindikwi Mkubulo na William Masai, waliipongeza hatua ya Waziri Magufuli kuhakikisha mhusika wa tukio hilo anakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia kama hizo.
Juhudi za NIPASHE kumpata muuguzi huyo ili kuzungumzia tukio hilo la aina yake katika fani ya utabibu hazikuzaa matunda jana.

Tuesday, November 27, 2012

Wanafunzi wamlipua Mkurugenzi Ustawi wa Jamii

Serikali imeombwa kumwondoa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Mbonimpaye Mpango kwa madai kwamba anawashawishi wanafunzi kumkataa Mkuu wa Chuo hicho, Abuu Mvungi.

Ombi hilo lilitangazwa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Frank Nkinda, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Alisema kumekuwa hakuna maelewano mazuri kati ya Mkurugezi na Mkuu wa chuo kitendo ambacho kinawaumiza wanafunzi.

“Sisi Wanafunzi tunatamka Mpango maarufu kama mama mpango kuondoka chuoni hapa kwa kuwa amekuwa mwiba na chanzo cha migogoro,” alisema Nkinda.

Alisema Mpango amekuwa akikwamisha shughuli za wanafunzi kwa kupandisha ada kiholela kwa lengo la kuifanya Taasisi ikose wanafunzi ili utendaji wa Mkuu wa taasisi uonekane mbovu.

Nkinda alisema kutokana na hila hizo Mkurugenzi huyo amekuwa akipeleka taarifa za uongo serikalini kuwa wanafunzi hawamtaki mkuu, kumbe yeye ndiye mwenye matatizo ya kutoelewana naye.

NIPASHE ilimtafuta Mkurugezi wa Chuo hicho kwa njia ya simu ili kujua juu ya tuhuma hizo, simu haikupokelewa wala ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa.

NIPASHE ilipomtafuta Mkuu wa Chuo hicho simu zake zote za mkononi hazikupatikana.

Yanga kwenda Uturuki Des. 27





Uongozi wa klabu ya Yanga umesema timu yao itaondoka nchini Desemba 27 mwaka huu kuelekea Uturuki ambako itaweka kambi yake kujifua kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano ya klabu hiyo, Abdallah Bin Kleb aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kocha wa timu hiyo, Mholanzi Ernie Brandts kutoa pendekezo hilo.

Alisema kuwa kamati yake baada ya kukaa na kujadiliana na kocha huyo, imeamua timu ikaweke kambi ya mafunzo nchini humo kwa kipindi cha wiki mbili na kwamba kocha amewaambia nchi hiyo hutoa huduma bora za kambi za michezo.

“Timu yetu imeanza mazoezi rasmi leo (jana) asubuhi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na mashindano ya Kombe la Kagame yatakayoanza mwezi Januari mwakani,” alisema Bin Kleb.

“Hii itatoa fursa kwa wachezaji wote kujumuika pamoja kwani kwa sasa baadhi ya wachezaji wetu wapo wanazitumikia timu zao za taifa kwenye mashindano ya Chalenji nchini Uganda.

“Hivyo mara tu mashindano ya Chalenji yatakapomalizika, watarejea nchini kujiunga na mazoezi na wachezaji wenzao tayari kujiandaa na safari hiyo… kocha ana uzoefu na nchi ya Uturuki, hivyo kwa mapendekezo yake, tulimkubalia na kuanza kuandaa maandalizi ya kambi hiyo lengo ikiwa ni kuifanya timu yetu icheze soka safi la burudani na ushindi.”

Mwenyekiti huyo ambaye pia alifanikisha usajili wa Mrwanda mwenye asili ya Kongo, Mbuyu Twite, alisema kuwa wakiwa Uturuki, watacheza mechi mbili za kirafiki na timu za nchi hiyo ambazo hata hivyo hakuzitaja.

Aidha, Bin Kleb alisema kuwa wamepokea mapendekezo ya kocha wao kuhusu wachezaji wanaopaswa kubaki, kuondolewa na kusajiliwa wakati wa ‘dirisha dogo’ la usajili litakalofungwa Desemba 25 mwaka huu na watalitolea ufafanuzi baadaye suala hilo.

“Hatupendi masuala ya kukurupuka kutangaza vitu ambavyo havijakamilika, ndiyo maana hata usajili wetu uliopita tulitangaza baada ya kukamilisha kila kitu,” alisema.

Kuhusu kutakiwa na klabu za nje kwa wachezaji wao wawili, kiungo Mrwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na mshambuliaji Didier Kavumbagu raia wa Burundi, Bin Kleb alisema bado wanafanya mazungumzo na klabu hizo.

Fabregas anatakiwana klabu ya El Merreikh ya Sudan wakati Kavumbagu anayeongoza kwa magoli msimu huu, ametengewa dola za Marekani 10,000 na klabu moja ya Qatar ili aondoke Jangwani.

Katika hatua nyingine, Bin kleb alisema kuwa klabu hiyo itamtangaza afisa habari mpya wa klabu hiyo atakayerithi mikoba ya Louis Sendeu kabla ya Desemba 15 mwaka huu.

“Tunatambua umuhimu wa kuwa na afisa habari wa klabu yetu. Tutamtangaza kabla ya Desemba 15 na ripoti kamili kuhusu masuala mbalimbali ya Yanga tuitoa Desemba 8 mwaka huu wakati wa Mkutano Mkuu na wanachama wa klabu hii,” alifafanua zaidi Bin Kleb. 

Licha ya kuanza ligi vibaya kwa vipigo viwili na sare moja katika mechi nne za kwanza hadi kufikia kumfukuza kocha aliyewapa ubingwa wa klabu bingwa Afrika Mashariki (Kombe la Kagame), Mbelgiji Tom Saintfiet, waliyedumu naye kwa siku 80 tu, Yanga walimaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni kwa pointi 29 wakifuatiwa na Azam (24) na Simba (23).

Radi yaua watatu wakisali chini ya mti

Watu watatu wamekufa papo hapo wawili wa familia moja na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na radi wakati wakifanya ibada chini ya mti katika kitongoji cha Mtakuja, kijiji cha Kivingo, kata ya Longuza, wilayani hapa.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 10:30 jioni huku kukiwa na upepo mkali uliombatana na manyunyu ya mvua.

Afisa Tarafa ya Umba, Mpemba Gabriel, aliwataja waliokufa kwa kupigwa na radi hiyo kuwa ni Esther Moleto, Salome Sengasu na ndugu yake Naiyo Sengasu.

Gabriel alisema kuwa majeruhi wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Mnazi kwa matibabu.

“Walikuwa chini ya mti wakiendelea na ibada ghafla hali ya hewa ilibadilika na kuibuka upepo mkali ulioambatana na mvua,” alisema Gabriel.

Naye Afisa Tarafa ya Mlalo, Dunstan Mudu, alisema kuwa kabla ya tukio hilo kulikuwa na ngurumo za radi zilizoambatana na upepo mkali.

Mudu alisema hali hiyo iliwatisha wakazi wa maeneo hayo na kulazimika kuacha shughuli zao kisha wakajifungia ndani ya nyumba zao.

Kufuatia tukio hilo, viongozi wa serikali wa ngazi za kata, tarafa hadi wilaya ya Lushoto, wamewashauri wananchi kutokaa karibu na miti wakati mvua zinaponyesha.

Alisema wilaya ya Lushoto imezungukwa na milima na misitu ya asili ambayo ni kichocheo kikubwa cha radi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Kata ya Longuza, Sadick Singano, alisema wilaya ya Lushoto imezungukwa na milima mingi huku makazi ya watu yakiwa chini.

Sungano alisema kuwa kwa kawaida radi hufuata miti na kuwataka wanaolima mabondeni kuwa makini kwani lolote linaweza kutokea.

Amuua mama yake kwa kumpiga mateke

MKAZI wa Swaya, jijini Mbeya, Ndele Julius, anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi kwa kumpiga mateke na ngumi. Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, iliyotumwa kwa waandishi wa habari jana, ilieleza kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 25, mwaka huu, eneo la Swaya. Taarifa hiyo ilimtaja mwanamke huyo aliyeuawa kuwa ni Sinjembele Julius (62), aliyekuwa mkulima. “Chanzo cha kifo hicho ni mtuhumiwa kuwa na ugomvi na kijana mwenzake ndipo mama yake alipokwenda kuamulia ugomvi na kugeukwa na mwanaye kisha kuanza kushambuliwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. Ilielezwa kuwa baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa huyo alikimbia, hivyo Jeshi la Polisi linatoa wito kwa mtu au watu wenye taarifa juu ya mahali alipo mtuhumiwa, ili akamatwe au ajisalimishe mwenyewe.

Monday, November 26, 2012

Sharo Millionea amefariki katika ajali

HABARI ZISIZOTHIBITISHWA ZILIZOTUFIKIA HIVI PUNDE: Msanii mahiri wa uchekeshaji na mwanamuziki wa Bongo Fleva Sharo Millionea amefariki katika ajali ya gari huko Muheza mkoani Tanga. Tutaendelea kuwajulisha kadiri tutakavyopata habari zaidi.

Wasanii wa bongo move 'Mlopelo' na John Maganga kufariki dunia wiki hii.

TASNIA ya filamu nchini imeendelea kukumbwa na simanzi baada ya wasanii wawili, Halid Mohamed maarufu kama 'Mlopelo' na John Maganga kufariki dunia wiki hii.Baada ya Mlopelo kuzikwa juzi, habari nyingine zilizopatikana jana ni kufariki kwa msanii Maganga katika hospitali ya Muhimbili juzi.

Rais wa Shirikisho la Sanaa Tanzania, Jacob Steven JB alithibitisha kutokea vifo hivyo na kusema wamepoteza watu muhimu kwenye sanaa ya filamu.
"Tunasikitika kutokea kwa vifo vya wasanii wenzetu. Walikuwa na mchango mkubwa katika kuisukuma sanaa hii kwenda hatua ya mafanikio," alisema JB.

"Wasanii wote tupo kwenye maombolezo makubwa na tunawapa wafiwa wote pole kutokana na misiba hii," alisema zaidi JB.

JB aliongeza kuwa taarifa kuhusu ratiba ya Maganga zitatolewa na uongozi wao wa juu.
Taarifa za awali zinadai kuwa Maganga alifariki baada ya kuumwa tumbo na kuwahishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kufariki usiku wa kuamkia jana.

'Man City, Chelsea mechi tamu leo'

LONDON, England
KAULI ya Kocha Rafa Benitez kwamba kama angependekezwa kufundisha Chelsea, kwenye orodha ya makocha angesimama mwisho, leo inaweza kuzua jambo mbele ya mashabiki wa timu ya Chelsea aliyopewa jukumu la kuifundisha atakapowavaa mabingwa watetezi England, Manchester City.

Ni mtihani wa kwanza kwa Benitez tangu atwae mikoba ya kufundisha Chelsea, mabingwa hao wa Ulaya Jumatano iliyopita akichukua nafasi ya Kocha Roberto Di Matteo.

Benitez ana historia na mashabiki wa Chelsea, siyo kwa sababu yeye ni mtu anayeonekana anaweza kumfunika rekodi ya Kocha Jose Mourinho, bali namna alivyowahi kuwazungumzia.
Aliiongoza kwa mafanikio Liverpool na sasa ana Chelsea mpya yenye wachezaji kama Juan Mata, Oscar na Eden Hazard, ambao hawana mbinu za kuzuia na kuharibu.

Ni wazi kabisa, mashabiki wa Chelsea siyo rahisi kuvutiwa sana na Rafa, lakini wana mtu mwingine wa kuvutiwa naye. Huyu ni Brendan Rodgers.Kocha wa City, Roberto Mancini anaamini Chelsea itakuwa hatari zaidi baada ya kumwondoa Kocha Roberto Di Matteo.
Mabingwa hao watetezi wanakwenda Darajani leo kuikabili Chelsea itakayokuwa na kocha wa muda akiiongoza The Blues mara ya kwanza ndani ya siku tano tangu kupewa jukumu hilo.
Mancini, anayeamini kuwa Di Matteo hakuwa na bahati kwenye kazi yake, anasema Chelsea inaweza kufaidika kimchezo kutokana na mazingira ya kocha mpya.

"Kwa kawaida, timu inapobadilisha kocha, upande wa upinzani wanaocheza nao huwa mgumu," alisema Mancini. "Kwetu nadhani ni ngumu sana."
Mancini amesikitishwa kwa kocha mwenzake raia wa Italia kutimuliwa kazi, ambaye alikutwa na panga hilo baada ya The Blues kunyukwa mabao 3-0 na Juventus kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa.

"Nimesikitika kuondoka Di Matteo, yeye alishinda taji la Mabingwa wa Soka Ulaya miezi sita iliyopita. Siku zote maisha huwa hivyo" aliongeza.
"Tunapokuwa na chaguo la kazi hii, pia tunafahamu kwamba kwenye maisha lolote linaweza kutokea."
City wameipindua Chelsea kileleni mwezi huu na sasa wanaongoza msimamo, lakini bado anaamini kuwa wapinzani wao walikuwa wazuri chini ya Di Matteo.
"Kabla ya mechi tatu za mwisho, walionyesha mchezo mzuri na walikuwa kileleni mwa msimamo," alisema.

"Bado naamini Chelsea walikuwa wazuri chini ya Di Matteo na itakuwa timu nzuri zaidi ikiwa na Benitez. Wana wachezaji wazuri zaidi."
Benitez anaungana na mshambuliaji wake aliyemsajili na kumwacha Liverpool kabla ya kujiunga na Chelsea, Fernando Torres, ambaye Di Matteo alimweka benchi kwenye mechi ya Turin dhidi ya Juventus Jumanne iliyopita.

Torres amefunga mara moja tu katika mechi tatu za mwisho na Mancini anaongeza: "Nadhani Fernando ni mshambuliaji mzuri. Wakati mwingine ni vigumu kwa mshambuliaji kama hafungi mabao kama alivyo yeye."

Wanawake 517 wanauawa kikatili kila mwaka

Wanawake 517 huuawa kila mwaka nchini kwa imani za kishirikina na 24 kati ya hao ni wa kutoka Mkoa wa Singida.

Mratibu wa Kanda ya Kati wa Mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayopinga ukatili wa kijinsia (Mkuki), Sara Mwaga, aliyasema hayo katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia Duniani.

“Taarifa za kitaifa za polisi kwa mwaka 2009/2010 zinaonyesha kuwa wanawake 517 huuawa kila mwaka kwa imani za kishirikina na 24 kati ya hawa ni wa kutoka Mkoa wa Singida,” alisema.

Mwaga alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanyika na Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) wa mwaka 2010 unaonyesha kuwa moja kati ya kila wanawake nchini wameshawahi kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono maishani mwao.

Pia alisema utafiti huo umeonesha kuwa asilimia 10 ya wanawake nchini walifanya kitendo cha kujamiana kwa mara ya kwanza kwa kulazimishwa na si kwa hiari yao.

“Utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 39 ya wanawake nchini wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo,” alisema Mwaga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la AFNET.

Aidha, alisema maadhimisho ya kitaifa yatafanyika mkoani Singida kwa mwaka huu na yanaratibiwa na shirika la Msaada wa sheria (WILDAF) kwa kushirikiana na Shirika la Action Aid chini ya Mtandao wa mashirika yanayopinga ukatili wa kijinsia nchini Mkuki.

Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ni Funguka, Komesha ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na sote tuwajibike.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma,  Gerimana Orotha, alisema bado ziko changamoto nyingi katika utekelezaji wa sheria dhidi ya ukatili wa kijinsia, ikiwemo rushwa, ukosefu wa vitendea kazi na umbali wa huduma muhimu hasa miundombinu mibovu hasa vijijini.

“Lakini ndio maana tumeruhusu wadau mbalimbali wakiwemo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuchangia juhudi hizi, na kuziba baadhi ya mapengo yaliyojitokeza,” alisema.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, Ismail Kaitila, alisema matukio mengi ya ukatili wa kijinsia hutokea katika kipindi cha kiangazi

Mwalimu adaiwa kumuua mwanafunzi wake kwa kisu

Mwalimu wa Shule ya Msingi Kwamwachalima iliyopo katika kijiji cha Kwamwachalima, kata ya Komkonga, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Nangoma Suhalungi Nangoma (23), anatuhumiwa kumuua kwa kisu mwanafunzi wake na kumjeruhi mwingine.

Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, polisi wanamtafuta mtuhumiwa huyo ili afikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

Mwalimu huyo anadaiwa kumuua mwanafuzi wa darasa la tatu katika shule hiyo.

Kadhalika, mwalimu huyo anakabiliwa na tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kisaza iliyopo katika kata hiyo.

Habari kutoka katika eneo la tukio ambazo zimethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, zilieleza kwamba tukio hilo lilitokea Novemba 23, mwaka huu saa 9:00 usiku baada ya muuaji kuwavamia watoto hao chumbani kwao na kuwachoma kisu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huku akiwa na huzuni shuleni hapo, baba wa marehemu, Ijumaa Mjaliwa, alimtaja binti yake aliyepoteza maisha kuwa ni Farihia Mjaliwa (9) na aliyejeruhiwa ni Mohamed Mjaliwa (16).

Mohamed ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Sekondari ya Kisaza.

“Aliyemuua mwanangu na kumjeruhi kijana wangu ni Mwalimu mwenzangu ambaye tunafundisha wote hapa shuleni. Alimchoma kisu kifuani eneo la moyoni. Sina ugomvi naye na tunakaa nyumba moja ila usiku mimi sikulala hapa,” alisema Mjaliwa na kuongeza:

“Yeye alikuwa na kesi ya kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili, hivyo alikuwa nje kwa dhamana, jana walimu wote tulifanya kikao cha kujadili namna ya kumuwekea dhamana mahakamani, maana kesho yake kulikuwa na taarifa kwamba angepelekwa mahakamani kujibu mashitaka hayo, ila yeye katika mkutano huo hakuwapo.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo, Ali Hatibu, alisema walimhoji majeruhi huyo kabla hajapoteza fahamu na kumtaja mwalimu huyo kwamba ndiye aliyewachoma kisu pamoja na marehemu.

“Tuliingia chumbani kwa watoto na kukuta damu lakini pia binti huyu ambaye sasa ni marehemu, tulimkuta akiwa tayari amekufa huku akiwa ameshika kisu. Amechomwa kwenye moyo akakiacha mwilini, binti akakichomoa na kupoteza maisha muda huo huo, yaani tukio hili linasikitisha sana maana mtoto hakujua kinachotokea,” alisema Hatibu.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Eva Msenga, alisema siku ya tukio majira ya mchana, alimhoji mwalimu huyo kutokana na mwenendo wake kuonekana si wa kawaida, na kumjibu kwamba amechanganyikiwa kutokana na suala linalomkabili la kufikishwa mahakamani, hivyo alimtaka afike ofisini kwake ajieleze.

“Mimi nilikuwa na watoto hawa usiku hadi saa tatu, wakijisomea nikawaambia wakalale kwa kuwa muda wa kupumzika ulikuwa umefika, wakaenda kulala baadaye usiku wa manane ndipo mtuhumiwa akabisha hodi na kufunguliwa kisha akaanza kufanya ukatili huo wa kutisha,” alidai Msenga.

Akizungumza wakati akiwafariji familia iliyokumbwa na mkasa huo shuleni hapo, Mkuu wa wilaya hiyo Rweyemamu, aliwataka wananchi kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu, akisema kwamba serikali imeanza kumchukulia hatua mwalimu huyo kwa kufunga akaunti yake benki.

Rweyemamu ameomba vyombo vya habari kusaidia kumfichua mtuhumiwa huyo ambaye ni mwenyeji wa mikoa ya Kusini ili sheria ifuate mkondo wake.

“Atakamatwa tu, tutafanya kila namna kwa kuchukua hatua aina zote kuhakikisha kwamba mwalimu huyu anakamatwa ili apambane na mkono wa sheria,” alisema Rweyemamu ambaye alifuatana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Aziz Kimata.

Mwili wa marehemu huyo ulisafirishwa kupelekwa Chalinze wilayani Bagamoyo na mazishi yalitarajiwa kufanyika jana eneo hilo.

Njaa yatesa wanafunzi Maswa

ZAIDI ya robo tatu ya wanafunzi katika shule za msingi wilayani Maswa, mkoa wa Simiyu, hushinda bila kupata mlo wa mchana wala maji ya kunywa wawapo shuleni na kusababisha kiwango cha ufaulu kushuka.
Tatizo hilohilo pia huwakumba walimu wa shule hizo kutokana na kuishi mbali na makazi yao kutokana na shule nyingi kutokuwa na nyumba za walimu.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Luten mstaafu Abdallah Kihato, alipokuwa akizungumzia changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ya msingi wilayani hapa na kusababisha kuwepo kwa mdololo mkubwa wa ufaulu na kuwapo kwa wimbi kubwa la utoro.
Alisema shule nyingi wilayani humo hazina huduma ya chakula kwa wanafunzi wake na imekuwa sababu kubwa inayochangia kushuka kwa taaluma na kiwango cha utekelezaji wa mitaala na kusababisha kiwango cha utoaji wa elimu ya msingi kuwa chini ya wastani wa asilimia 50.
Kutokana na hali hiyo, aliwashauri madiwani wa halmashauri hiyo kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata angalau mlo wa mchana na majisafi wawapo shuleni.

Saturday, November 24, 2012

 
Ni pengo lingine katika tasnia ya film (bongo movie),,,ndugu yetu,,rafik yetu na pia mtanzania mwenzetu,,,JOHN STEPHANO....Amefarik dunia mungu ailaze roho ya marehem mahali pema pepon ""Amin

Friday, November 16, 2012

Tanzania na Malawi wajadili mpaka wa Ziwa Nyasa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John M. Haule, akifungua Mkutano wa Timu ya Pamoja ya Wataalam kati ya Tanzania na Malawikuhusu mgogoro wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa. Mkutano huo uliowahusisha wataalam kutoka Wizara na Idara mbalimbali za Serikali za Tanzania na Malawi unafanyika Jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Serena.
Bw. Julius Chisi, Naibu Mpimaji Ardhi Mkuu kutoka Malawi akizungumza machache wakati wa mkutano huo.
Bw. Abdallah Mtibora, Afisa kutoka Kitengo cha Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kufungua mkutano huo.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Tanzania akiwemo Mhe. Balozi Patrick Tsere (wa pili kutoka kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Malawi na Balozi Irene Kasyanju (kushoto) wakimsikiliza Bw. Chisi (hayupo pichani) wakati wa akizungumza.
Baadhi ya Wajumbe wengine kutoka Malawi akiwemo Mhe. Chiyaonga (kulia), Balozi wa Malawi hapa nchini.
Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Malawi wakimsikiliza Katibu Mkuu (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John M. Haule akizungumza na Mhe. Flosie Gomile Chiyaonga, Balozi wa Malawi hapa nchini kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Timu ya Pamoja ya Wataalam wa Tanzania na Malawi kuhusu mgogoro wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa.Picha na Habari- Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa – Mkutano kati ya Tanzania na Malawi kujadili suluhu ya mgogoro wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa umeanza katika ngazi ya Wataalamu jijini Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2012. Mkutano huo unaowahusisha wataalam kutoka Wizara na Idara mbalimbali za Serikali za Tanzania na Malawi unafanyika Jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Serena. Akifungua Mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John M. Haule alisisitiza umuhimu wa wajumbe kutoka nchi zote mbili kujadili na kupendekeza njia zitakazosaidia kupata suluhisho la kudumu la mgogoro huo. Aidha, Bw. Haule aliweka bayana kuwa Serikali ya Tanzania ina dhamira ya dhati kufanya kazi pamoja na Serikali ya Malawi kutafuta suluhu ya mgogoro huo jambo ambalo pia lilisisitizwa na Bw. Julius Chisi, Kiongozi wa Ujumbe wa Malawi. Mkutano huo ambao utafanyika kwa siku tatu hadi tarehe 17 Novemba, 2012 umeanza na Kikao cha Wataalamu ambacho kitafuatiwa na kikao cha Maafisa Waandamizi na kuhitimishwa na kikao cha Mawaziri tarehe 17 Novemba, 2012.

Mgambo waua na kujeruhi Machinga kwa risasi Mwanza.

KWA mara nyingine tena, jiji la Mwanza limegeuka kuwa uwanja wa mapambano baada ya kuibuka mapigano makali baina ya mgambo na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga.
Katika mapigano hayo yaliyotokea jana majira ya saa tano asubuhi, polisi na mgambo hao walilazimika kutumia risasi za moto kujihami na hivyo kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyepigwa risasi na mgambo.
Mbali na kuuawa kwa mtu huyo, pia wengine wawili walijeruhiwa vibaya kwa risasi katika mapambano hayo yaliyofanyika kwenye makutano ya barabara ya Pamba, Miti Mirefu na stendi ya zamani ya Tanganyika iliyoko katikati ya jiji.
Chanzo cha vurugu hizo kinaelezwa kuwa ni mgambo wa jiji waliokuwa kwenye operesheni ya kuwaondoa Machinga hao kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kufanya biashara.
Ilielezwa kuwa mgambo hao walifika maeneo hayo ya barabara ya Pamba kisha kuanza kukamata bidhaa za Machinga na kuondoka nazo bila wahusika kuwakamata.
Mashuhuda walidai kuwa tukio hilo liliwapandishia hasira Machinga hao kisha kuanza kuwashambulia kwa mawe askari hao wa jiji ambao baadaye walilazimika kujihami kwa kufyatua risasi za moto zilizogharimu maisha ya mmoja wa Machinga hao maarugu kama ‘Chapombe’.
Msako huo ulidaiwa kufanywa kimya kimya na mgambo hao badala ya kutoa tangazo kwa wahusika kuondoka maeneo hayo kama sheria inavyosema.
“Mimi nimeshuhudia kabisa mgambo wa jiji wakichukua bidhaa za Machinga, baadaye Machinga nao wakakasirika na kuanza kuwarushia mawe, ndipo mgambo wakaanza kufyatua risasi wakiwalenga watu,” alisema shuhuda.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola, alithibitisha kuuawa kwa risasi mtu mmoja katika mapambano na kumtaja marehemu kuwa alikuwa mpiga debe.
“Leo zilizuka vurugu kubwa kati ya Machinga na mgambo wa jiji. Vurugu hizi zilitokea baada ya Machinga kumkimbilia na kumkwida mgambo shingoni kisha kumtolea sime.
“Baada ya kuona hivyo, mgambo waliokuwa kwenye operesheni walilazimika kujihami kwa kufyatua risasi hewani, lakini bahati mbaya ilimpata mpiga debe na kufa papo hapo na wengine wawili walijeruhiwa na wamelazwa Hospitali ya Bugando,” alisema Matola.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, alieleza kusikitishwa na vurugu hizo na kusema mgambo hao walikuwa kazini kama walivyopangiwa katika utaratibu wa kawaida.
Kwa mujibu wa Kabwe, utaratibu na sheria za jiji la Mwanza ni kuwaondoa Machinga katikati ya jiji na kwamba operesheni ya mgambo ya kuwaondoa Machinga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria bado inaendelea.
Hili ni tukio la tatu kwa pande hizo kuzua vurugu tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 na katika matukio yote watu walipigwa na kuuawa kwa risasi, jambo linalolalamikiwa na wananchi.
Polisi na ‘majambazi’
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi mkoani hapa, limewaua watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi katika tukio la kurushiana risasi usiku wa kuamkia jana katika Big Bite Kilimahewa Wilaya ya Ilemela.
Kamanda Matola aliwaambia waandishi wa habari kwamba tukio hilo lilitokea majira ya saa 5 usiku wa Novemba 14, mwaka huu, ambapo katika majibizano ya risasi na watuhumiwa hao watano, watatu walifanikiwa kukimbia huku polisi wakiwapokonya bunduki aina ya SMG na risasi 43.
Hili ni tukio la kwanza la polisi kurushiana risasi na majambazi tangu mauaji ya aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow, yaliyofanyika hivi karibuni.

Machinga mwingine amejeruhiwa kwenye mkono wa kushoto katika kiwiko, naye dereva wa magari ya biashara za kusafirisha mizigo wa gari aina ya Kenta, magari ambayo hupaki katika eneo hilo amejeruhiwa upande wa kushoto kichwani na kukimbizwa hospitali ya rufaa Bugando kwa matibabu.
Mkuu wa polisi (OCD) wa wilaya ya Nyamagana Ally Kitumbu. akizungumza na wafanyabiashara hao wadogo (wamachinga) kuendelea na kazi kwa kufuata sheria wakati jeshi hilo likifanya uchunguzi wa tukio hilo.
Mmoja wa viongozi wa akiwatuliza wamachinga wenzake kupata kumsikiliza mkuu wa polisi (OCD) wa wilaya ya Nyamagana Ally Kitumbu. .

Operesheni ya Magufuli magari ya serikali leo

Kikosi cha Usalama Barabarani, kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, leo kinafanya operesheni ya nchi zima ya kukagua magari ya umma yanayotumia namba za kiraia badala ya namba stahiki zinazotakiwa kutumika katika magari ya umma. Akizunguzna na NIPASHE ofisini kwake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alisema wanafanya operesheni hiyo kufuatia agizo alilolitoa Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli la kutaka magari yote ya umma yenye namba za kiraia, yarejeshwe kwenye namba stahiki za magari hayo. Kamanda Mpinga alisema baadhi ya vitu watakavyokuwa wanaangalia katika operesheni hiyo ni sehemu ya kioo cha gari pamoja na stika ya bima. “Inawezekana wengine wakaghushi namba, lakini tumejipanga, kuna vitu tutakuwa tunaangalia, kwa hiyo tutazibaini tu,” alisema. Dk. Magufuli aliwaagiza wale wote wanaotumia namba za kiraia katika magari ya umma, wawe wameyasajili katika namba stahiki na mwisho wa kutekeleza agizo hilo ilikuwa ni jana. Lengo la Dk. Magufuli kuanzisha operesheni hiyo ni kudhibiti matumizi mabaya ya magari ya umma yanayotumia namba za kiraia katika shughuli binafsi na hivyo kuisababishia serikali hasara. Dk. Magufuli alisema operesheni hiyo itahusisha magari yote ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala wa Serikali, Mashirika ya Umma na taasisi nyingine za umma na kwamba watawachukulia hatua walionunua magari hayo, lakini bado wanatumia namba zinazoonyesha kuwa ni milki ya serikali.

Muuguzi mbaroni kwa tuhuma za kuiba kichanga

Jeshi la Polisi la Mkoa wa Pwani, linamshikilia Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, Rehema Gogo (34) kwa tuhuma za kuiba kichanga cha siku moja.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Phransisco Mwamisi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

“Ni kweli kichanga hicho kiliibwa na muuguzi wa pale hospitali siku ya Novemba 10, mwaka huu, majira ya saa tano asubuhi,” alisema Mwamisi.

Alisema muuguzi huyo kwa sasa ameshikiliwa na Jeshi la Polisi tangu siku ya tukio.

Jeshi la Polisi Wilaya hiyo lilithibitisha kutokea wizi wa kichanga hicho.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, mtuhumiwa huyo, ambaye alikuwa likizo, alikodi gari na kwenda hospitalini hapo na kuingia katika wodi ya wazazi.

“Aliingia wodini humo na kuchukuwa kichanga na kumfunika kwenye hijabu yake. Mama wa mtoto huyo alikuwa ametoka nje kwenda kupiga simu kwao, kwani alijifungua usiku na aliporudi hakumkuta mtoto wake,” alisema mmoja wa maofisa waandamizi wa jeshi hilo wilayani humo.

Monday, November 12, 2012

Bomoabomoa Ubungo Kibangu kuanza leo

Nyumba zilizopo Ubungo Kibangu katika Kata ya Makubuli, jijini Dar es Salaam zitaanza kubomolewa kuanzia leo kwa lengo la kuendeleza mradi wa ujenzi wa barabara. Serikali kupitia Manispaa ya Kinondoni imeagiza kuwa wananchi na wafanya biashara walio katika eneo hilo waondoke kabla ya zoezi hilo kuanza. Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Dar es Salaam, na Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa, Desdery Ishengoma, wakati akizungumza na wakazi wa eneo hilo. Ishengoma alisema ujenzi huo unatarajia kuanza mara baada ya nyumba hizo kubomolewa. Alisema serikali ilishawalipa madai yao na ilitoa siku 60 kwa lengo la kuwataka waondokea katika eneo hilo na kutafuta maeneo mengine ya kuishi na kwamba baadhi ya watu walikwishaondoka kupisha mradi huo. “Kuanzia sasa hadi kufikia Jumatatu (leo) muda wowote tingatinga litapita kubomoa hizi nyumba zote zenye alama katika eneo hili kwa sababu muda uliotolewa umekwishamalizika na malipo walishalipwa na selikali,” alisema Ishengoma. Aliongeza kuwa barabara hiyo itawanufaisha wananchi wa eneo hilo kwa kupunguza msongamano pamoja na athari za mafuriko yanayotokea mara kwa mara kwa kujenga mifereji mirefu na mikubwa.

Askari wastaafu JWTZ watapeliwa Z`bar

Askari wastaafu 700 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), visiwani Zanzibar wametapeliwa na kuamua kupitisha azimio la kumshitaki aliyekuwa Mwenyekiti wa Muungano wao, (Muwawata), Sajuni Taji Mstaafu Asseyd Mayungi.
Wapinganaji hao wastaafu wametapeliwa mamilioni ya fedha zikiwemo ada za uanachama za kujiunga na muungano wao pamoja na fedha za gharama za kuanzisha vikundi vya wajasiriamali katika kupambana na ukali wa maisha baada ya kumaliza utumishi wa umma.
Hayo yamefahamika katika mkutano wa wanachama wa Muungano huo kutoka Mikoa mitano ya Zanzibar uliyofanyika Amani, Mkoa wa mjini Magharibi Kisiwani Unguja na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa muda wa Muwawata, Brigedia Jenerali Mstaafu Haroun Othmani.
Akisoma azimio la mkutano huo, Mwenyekiti wa Muwawata, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Sajenti Mstaafu wa JWTZ Miraji Kiongwe, alisema wanaunga mkono kuondolewa madarakani kwa Sajuni Taji mstaafu Mayugi kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za muungano huo.
“Mikoa mitano ya Zanzibar kama wanachama tunaunga aliyekuwa Mwenyekiti wetu Asseyd Mayungi kuondolewa uongozi kwa tuhuma za kuhusika na ubadhirifu wa fedha za Muwawata,” alisema Kiongwe.
Alisema baada ya wanachama kujadili kwa kina ripoti ya ubadhirifu wa fedha za Muwawata wamekubaliana kila kikundi cha ushirika kilichotapeliwa fedha kufungua kesi haraka dhidi ya Mayungi na watu alioshirikiana nao kufanikisha mpango huo.
Kiongwe alisema Mayungi anatuhumiwa kuzunguka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar na kukusanya mamilioni ya fedha kama ada za kujiunga na Muwawata pamoja na fedha za kusajili vikundi vya Ushirika vya askari wastaafu kabla ya kupatiwa mikopo.
Alisema kwamba kazi hiyo alikuwa akiifanya kwa kushirikiana na Taasisi moja ya kusadia Wajasiriamali (jina lake linahifadhiwa) ambao walifika Zanzibar na kufanikiwa kukusanya fedha kutoka vikundi 18 vya ushirika.
Alisema Mayungi kwa kushirikiana na Taasisi hiyo jumla ya Sh. 23,880,000 zimekusanywa na kutumika tofauti na malengo ya Muwawata.
Kiongwe alisema kwamba tangu kukusanywa fedha hizo mwaka jana wamekuwa wakifuatilia maendeleo ya mikopo bila ya mafanikio kwa Taasisi hiyo ya kusaidia wajasiriamali na kubainika kuwa tayari wametapeliwa.
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Kamati ya mpito ya Uongozi wa Muwawata, Brigedia Jenerali Mstaafu Othman, aliwataka wanachama wa Muungano huo kuwa na moyo wa subira wakati tatizo hilo likishughulikiwa na uongozi wa mpito kabla ya wahusika kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Hata hivyo aliwataka kuendelea kuunga mkono viongozi walichaguliwa kwa muda kuongozi ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwa Muungano huo yanafanikiwa na kuwanufaisha wanachama wake.
Juhudi za kuwapata Asseyd na Taasisi ya kusaidia wajasiriamali ambazo zimekubwa na kashfa ya kuwatapeli wastaafu hao wa JWTZ hazikuweza kuifanikiwa kupitia simu zao za na barua pepe.

Sunday, November 11, 2012

Magu yaongoza mauaji ya vikongwe

WILAYA ya Magu iliyopo jijini Mwanza, imetajwa kuwa ni moja kati ya wilaya saba za jiji hilo zinazoongoza kwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), wazee na vikongwe.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili, wilaya hiyo imekuwa ni moja ya wilaya zinazoongoza kwa matukio ya mauaji ya vikongwe na watu hao wenye ulemavu wa ngozi, jambo linalokiuka haki za binadamu na utawala bora.
Takwimu za kiuchunguzi zinaonesha kwamba, tangu mwaka 2005 hadi Septemba 2012, idadi ya vikongwe waliouawa walikuwa ni 267, wakati albino waliouawa walifikia 68.
Akithibitisha kuwepo kwa tatizo hilo la mauaji hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jacqueline Liana, alisema licha ya kuwepo kwa mauaji hayo, lakini serikali imeweka mikakati ya kumaliza tatizo hilo huku watuhumiwa wa mauaji hayo wakikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Mkuu huyo wa wilaya alisema mauaji hayo yanasababishwa na visa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na imani za kishirikina, ambapo hadi sasa watu 2,183 walishakamatwa na kuhojiwa kutokana na kudaiwa kuhusika katika mauaji hayo na 1,599 walifikishwa mahakamani.
Alisema kutokana na matukio hayo serikali imekuwa ikijitahidi kuchukua hatua za kuwakamata watuhumiwa wanaofanya vitendo hivyo, lakini jamii imekuwa kikwazo kwa kushindwa kutoa ushahidi pindi unapohitajika.
Liana alisema kuwa watu wengi wamekuwa waoga wa kutoa ushirikiano kwa viongozi na vyombo vya dola kwa kuwa wengi wana imani ya kwamba endapo watatoa ushahidi ndugu wa watuhumiwa wanaweza kuwaua, huku uelewa mdogo ukichangia kuwepo kwa tatizo hilo.
“Kwa huku kwetu Magu ipo hofu miongoni mwa jamii kuwa ukisimama mahakamani ukatoa ushahidi, kama kuna mianya ya rushwa kati ya hakimu na mtuhumiwa, basi shahidi anaweza kugeukwa na akatupwa jela kwa kusingiziwa kutoa ushahidi wa uongo,” alisema.

Wednesday, November 7, 2012

Barack Obama na makamu wake Joe Biden wapongezana.

Rais Barack Obama na makamu wake Joe Biden wakiwa na wake zao wakipongezana baada ya Rais Barack Obama kutangazwa mshindi wa Urais wa nchi ya Marekani baada ya mbio za kampeni zilizokua zikiendelea takribani miezi kadhaa nyuma kuishia jana kwaRais Barack Obama kuibuka mshindi dhidi ya Gavana Mitt Romney wa Massachusetts.

Tuesday, November 6, 2012

Askofu Balina afariki.

ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Aloysius Balina, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza. Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Antony Makunde, imesema kuwa Askofu Balina amefariki jana mchana, kutokana na maradhi ya saratani ya ini kwa muda mrefu. Padre Makunde alisema kuwa, mapema mwaka huu, Askofu Balina alipelekwa Ujerumani kwa matibabu, na akarejea nchini akiwa mwenye afya njema. Hata hivyo, miezi michache alianza tena kusumbuliwa na ugonjwa huo, na afya yake ilizidi kudorora ambapo mwezi uliopita, alilazwa katika Hospitali ya Bugando kabla ya kufikwa na umauti jana. Askofu Balina alizaliwa Juni 21,1945, Ntuzu, Bariadi mkoani Shinyanga. Baada ya kuhitimu masomo yake mbalimbali, alipewa daraja la upadri Mei 26, 1971. Kutokana na utumishi wake mwema, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua kuwa askofu wa Jimbo la Geita mwaka 1985. Septemba 1997, aliteuliwa kuwa askofu wa Jimbo la Shinyanga ambako alilitumikia hadi jana alipoitwa na Mungu. Wakati wa uhai wake, Askofu Balina alishikilia nafasi kadhaa ndani ya Baraza la Maaskofu ambako kwa miaka mingi alikuwa mwenyekiti wa idara ya afya ya baraza hilo, na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Bugando. Askofu Balina ni mmoja wa maaskofu wachache wa Kikatoliki ambaye alitazama maisha ya waamini wake na watu wote wa majimbo ya Geita na Shinyanga, katika mahitaji yote ya kiroho na kimwili. Aidha, ni mmoja wa viongozi wa dini aliyesimamia kikamilifu kuinua Hospitali ya Bugando na hasa juhudi zake zilizosukuma kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Afya Bugando. Kadhalika, alifanya kazi kubwa akishirikiana na maaskofu wenzake, kuhakikisha kuwa kinaanzishwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine, na hatimaye kufikia mafanikio makubwa.

Mwanamke auawa, azikwa chooni

NGOLO Soni (45) mkazi wa kijiji cha Jihu, kata ya Badi, wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, ameuawa kwa kunyongwa na kisha mwili wake kuzikwa katika shimo la choo kijijini humo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na diwani wa kata hiyo, Martine Masele (CHADEMA), na kuthibitishwa na polisi wilayani Maswa, tukio la kuuawa kwa mwanamke huyo lilitokea Novemba 4 mwaka huu. Taarifa hizo zinaeleza zaidi kuwa kabla ya kugundulika kwa mauaji hayo, marehemu alikuwa akiishi peke yake na kutoweka nyumbani kwake tangu Oktoba 2, mwaka huu, hadi mwili wake ulipopatikana siku ya tukio. Awali ilidaiwa kuwa marehemu alikuwa akifanya biashara ya kununua mifugo na kuiweka kwa kaka zake ambao wanadaiwa kufanya unyama huo. Katika taarifa hiyo Masele alisema mara baada ya kumuua kwa kushirikiana walimzika marehemu katika shimo la choo nyumbani kwa rafiki yao aliyetajwa kwa jina moja la Zabron kijijini humo kwa miadi ya kumpatia sh milioni sita. Alisema walishindwa kutimiza ahadi yao na hivyo siri ya mauaji hayo kuvuja na taarifa kutolewa jeshi la polisi wilayani hapa ambalo liliufukua mwili wa marehemu. Kutokana na mauaji hayo, Jeshi la Polisi Maswa linawashilikia watu wanne wakiwemo kaka wa marehemu ambao ni Wilson Soni (45), Majilia Soni (42) na Mbilo Soni (32) pamoja na rafiki yao Zabron na wote watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika wa mauaji hayo.

Hatimaye Obama kutikisa Marekani.

 Barack Obama amechaguliwa tena kuwa rais wa Marekani kwa amamu ya pili katika uchaguzi uliofanyika kuanzia jana.Hongera kwake.
 
kwa mara nyingine Barak Obama kupata ushindi kwa kishindo kikubwa sana na ndiye Rais wa kwanza Marekani kuwa mweusi na kashinda kwa kura 290 na mpinzani kuwa na kura 203.huku sherehe za kumpongeza obama zikiendelea huko nnchini marekani

Mwanafunzi achomwa kisu kwa wivu wa mapenzi

MWANAFUNZI wa Chuo cha Utalii cha Musoma Rose Kanyambo (21) ameshambuliwa kwa kisu na John Ogola anayesemekana alikuwa mpenzi wake na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili.
Tukio hilo lilitokea Novemba 2 mwaka huu saa mbili asubuhi katika bweni la chuo hicho lililoko mtaa wa Kamnyonge, manispaa ya Musoma.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alisema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi.
Alisema aliyejeruhiwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Ogola ambaye pia ni mwanafunzi wa chuo hicho lakini baadaye waliachana na Rose kuanzisha uhusiano na mwanaume mwingine.
Kamanda Mwakyoma alisema mtuhumiwa aliona kuwa hakutendewa haki kutokana na kwamba alikuwa akimgharamia msichana huyo kwa kila alichotaka na ndipo akaamua kumchoma kwa kisu mgongoni na ubavuni hali iliyomsababishia maumivu makali na kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Mara kwa matibabu.
Akizungumza hospitalini hapo Rose alisema kabla ya tukio hilo Ogola alikuwa akimfuata mara kwa mara akimshawishi awe mpenzi wake.
“Alikuwa akinisumbua mara kwa mara akinitaka nikubali kuwa mpenzi wake lakini mara zote nilikuwa nikimkatalia ombi lake ndiyo maana ameamua kunichoma kisu,” alisema Rose.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho walisema kuwa Rose na Ogala walikuwa katika mahusiano ya kimapenzi kwa muda mrefu na kwamba Ogala ndiye aliyekuwa akimgharamia Rose mahitaji yake.
Mtumiwa amekamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamni mara uchunguzi utakapokamilika.

Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Soraga amwagiwa tindikali.

Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga akitolewa katika Chumba cha Huduma ya Mwanzo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja baada ya kurushiwa Tindi kali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazowezi huko katika Kiwanja cha Mwanakwerekwe.
Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga akipandishwa kwenye Gari ya Wagonjwa kwa lengo la kuwahishwa katika Hospitali ya Muhimbili Dare es Salaam baada ya kurushiwa Tindi kali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazowezi huko katika Kiwanja cha Mwanakwerekwe.
Wananchi mbalimbali wakishuhudia Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga akiwahishwa katika Hospitali ya Muhimbili Dare es Salaam baada ya kurushiwa Tindi kali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazowezi huko katika Kiwanja cha Mwanakwerekwe.Picha na Yussuf Simai-Maelezo Zanzibar

Sunday, November 4, 2012

Kocha Yanga aisifu Azam

Kocha wa Yanga Ernest 'Ernie' Brandts amekisifu kikoisi chatimu ya Azam FC watakachokutana nacho kesho kwenye mchezo wa ligi kuu ya Bara kuwa kina wachezaji wenye uwezo mkubwa.
Akizungumza kwenye uwanja wa Azam Complex mara baada ya mchezo kati ya Azam na Coastal Union juzi, Brandts alisema licha ya Yanga kuwa kwenye kasi kwa sasa, watakuwa na kazi ngumu mbele ya timu hiyo.
"Nawafahamu Azam tangu kwenye mashindano ya Kombe la Kagame, na leo nimepata nafasi ya kuwaona tena," alisema Brandts na kueleza zaidi kuwa "ni timu nzuri na inayocheza soka la kisasa kwa sababu wachezaji wake wana stamina na wanacheza soka la nguvu.
"Kwa kweli tutakuwa na kazi ngumu kwenye mchezo wetu wa Jumapili (kesho)."
Aidha, alisema kuwa atatumia mapungufu aliyoyaona kwenye mchezo wa timu hiyo dhidi ya Coastal Union kuhakikisha kikosi chake kinapata matokeo mazuri kwenye mchezo wa kesho.
Alisema katika kikosi hicho cha Azam, ambayo juzi iliifunga Coastal 4-1, anamuhofia mshambuliaji John Bocco.
Aliema mchezaji huyo anajua kufanya kazi yake na kwamba kwake itakuwa furaha kama atakosekana kwenye mchezo huo.
Hata hivyo, habari ambazo Nipashe imezipata na kuthibitishwa na msemaji wa Azam, Jaffar Iddi, Bocco atakuwepo kikosini kesho baada ya kupona majeraha aliyoyapata kwenye mchezo wa kichapo cha magoli 3-1 dhidi ya Simba wiki iliyopita.
"Bocco anaendelea vizuri na hakuna shaka Jumapili (kesho) atakuwepo uwanjani kutegemea na kocha atakavyoamua... ila yuko vizuri baada ya kupona majeraha yake," alisema Iddi.
Kocha huyo wa Yanga alisema wachezaji wake kwa sasa wapo katika hali nzuri kimwili na kiakili; hasa baada ya kuibuka na ushindi mfululizo kwenye ligi kuu wakifuta machungu ya kuanza vibaya katika michezo minne ya mwanzoni mwa msimu.
Azam itaikaribisha Yanga kesho kwenye Uwanja Taifa, ukiwa ni mchezo wao wa kwanza wa timu hizo tangu mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati hao waifunge timu hiyo ya wauza vyakula 2-0 kwenye fainali ya Kombe la Kagame Julai.

Afisa Elimu avuliwa madaraka.

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, limemvua madaraka ofisa elimu wa shule za sekondari, Bilungama Nyalinga, kutokana na tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Akitoa taarifa ya kuvuliwa madaraka hayo wakati wa kikao cha baraza la madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Juma Maganga, alisema kuwa uamuzi huo umekuja baada ya tume kufanya uchunguzi wa kina juu ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili ofisa huyo.
Maganga alizitaja tuhuma zilizokuwa zikimkabili kuwa ni kutumia vibaya madaraka aliyokuwa nayo, matumizi mabaya ya fedha za ofisi, kuwa na mahusiano mabaya na walimu anaowaongoza, na kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani hapo.
“Nyalinga hatakuwa na cheo cha ofisa elimu katika wilaya hii kuanzia sasa, na anaruhusiwa kukata rufaa mahali popote tangu pale atakapokuwa amepokea barua ya kumtaarifu juu ya suala hili,” alisema Maganga.
Alisema kuwa kabla ya kuvuliwa madaraka, alisimamishwa kazi na baraza hilo kwa miezi mitatu iliyopita na kuundwa kwa tume ya uchunguzi iliyokuja na ripoti ya kubaini madudu hayo yaliyokuwa yakimkabili.

Mwanafunzi abakwa na kunyongwa

WATU wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti, mkoani Mara, akiwemo mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi aliyebakwa na kisha kunyongwa kwa kutumia gauni lake na watu wasiofahamika na mwili wake kutupwa kwenye pagale.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alisema kuwa matukio hayo yalitokea Agosti 30, mwaka huu katika maeneo tofauti mkoani humo.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa, katika tukio la kwanza, mwanafunzi mmoja aliyekuwa anasoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Makoko, aligundulika akiwa amekufa na kisha mwili wake kutupwa kwenye pagale eneo la Darajani.
Alisema kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi, pamoja na daktari ulionyesha kuwa mwanafunzi huyo alibakwa na kisha kunyongwa kwa gauni lake alilokuwa amevaa, na watu wasiojulikana.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa, kwa maelezo ya wazazi, binti huyo alitoweka nyumbani kwao siku mbili kabla ya mwili wake kuokotwa katika pagale.
Aidha, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo, ili wale waliohusika katika kufanya ukatili huo waweze kubainika na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika tukio la pili, mwanaume mmoja, Kizwere Ndege (47), aliyekuwa anatembea kwa miguu, amefariki baada ya kugongwa na basi la Kampuni ya Bunda Express, eneo la Iramba, Wilaya ya Butiama
Alisema kuwa basi hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva Ramadhan Karimu mkazi wa Mwanza, na kwamba chanzo cha ajali hiyo kinaelezwa kuwa ni mwendo kasi.

Sherehe ya kumuaga Luteni Jenerali mstaafu Abdulrahman Shimbo

Askari wa kikosi cha bendera kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakitoa heshima kwa mwendo wa haraka mbele ya Luteni Jenerali Mstaafu Abdulrahman Shimbo (hayupo pichani) wakati wa sherehe za kumuaga zilizofanyika leo katika kambi ya jeshi hilo Mgulani jijini Dar es Salaam. Luteni Jenerali Mstaafu Shimbo amelitumikia jeshi hilo kwa zaidi ya miaka 41 na kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mnadhimu mkuu wa Jeshi.
Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakitoa heshima kwa mwendo wa pole mbele ya Luteni Jenerali Mstaafu A Shimbo (hayupo pichani) wakati wa sherehe za kumuaga zilizofanyika leo katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mgulani jijini Dar es Salaam. Luteni Jenerali Mstaafu Shimbo amelitumikia jeshi hilo kwa zaidi ya miaka 41 kwa kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mnadhimu mkuu wa Jeshi.
uteni Jenerali Mstaafu Abdulrahman Shimbo (aliyesimama kwenye gari) akisindikizwa maafisa na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ikiwa ni kuhitimisha sherehe za kumuaga rasmi zilizofanyika leo katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mgulani jijini Dar es Salaam. Luteni Jenerali Mstaafu Shimbo amelitumikia jeshi hilo kwa zaidi ya miaka 41 kwa kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mnadhimu mkuu wa Jeshi.

Saturday, November 3, 2012

Siri nzito uhaba wa mafuta

  Waziri atangaza kufuta leseni za mafuta
  Mbunge CCM ataka `kuishughulikia` Serikali

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene
Hatma ya ukosefu wa mafuta nchini hususani ya dizeli na petroli imegubikwa na utata, kutokana na serikali kutoa taarifa zinazopingana.
Mazingira Wakati Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, akiliambia Bunge, mafuta yameanza kusambazwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imesema utekelezaji wake bado haujaanza.
wakati hali ikiwa hivyo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ametangaza kufutwa leseni za biashara ya mafuta kwa kampuni zilizokiuka taratibu.
Pia ameivunja bodi ya kampuni ya uingizaji mafuta nchini (PIC) kwa madai kuwa inaundwa na wajumbe walio wafanyabiashara ya mafuta wasiokuwa na uwezo katika sekta hiyo.
Lakini hali ilivyo sasa, mikoa kadhaa kadhaa imejikuta katika kadhia hiyo, hali iliyomsababisha Mbunge wa Mwibara (CCM), Alphaxard Lugora kulitaka Bunge lisitishe shughuli zake jana na kulijadili tatizo hilo.
Hatua ya Lugora imeilazimisha serikali kutoa tamko la awali bungeni, kupitia kwa Simbachawene, ikisema limeshaanza kushughulikiwa na hali imeanza kurejea kuwa ya kawaida.
Wakati Bunge likielezwa hivyo jana, Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, hali ya upatikanaji mafuta bado ni ngumu.
Katika tukio la bungeni, baada ya Spika Anne Makinda kumaliza matangazo jana asubuhi, Lugora alitumia kanuni ya 47 kutaka shughuli za Bunge zisitishwe, badala yake kujadiliwa hali ya dharura ya uhaba wa mafuta nchini.
Hoja hiyo iliungwa na wabunge wengi kupitia mfumo wa kusimama, ambapo walikuwemo wa CCM na wanaotokana na vyama tofauti vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akiwasilisha hoja hiyo, Lugora alisema upatikanaji wa nishati hiyo hususani dizeli na petroli ni mbaya kuliko maelezo.
Alisema sasa hivi imefikia hatua ambapo mteja akienda kununua bidhaa hiyo kwenye vituo vya mafuta, anapimiwa kwa `vibaba’. “Mimi mwenyewe niliambiwa nipewe lita 10 ili wengine waweze kupata,” alisema.
Alisema hali kama hiyo inaweza kuwatokea watu tofauti wakiwemo wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma ya gari maalum la kusafirishia wenye matatizo ya afya.
Lugora alisema kutokana na `unyeti’ wa jambo hilo, kuna wasiwasi wa kukwepo kwa hujuma kutoka kwa kampuni kubwa, ionekane Sheria ya Ununuzi wa Jumla (bulk procurement) imeshindikana hivyo kurejesha ununuzi wa rejareja.
Lugora aliomba wabunge wamuunge mkono hoja yake hiyo, ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo, ambapo idadi kubwa ya wabunge ilifanya hivyo.
Hata hivyo, serikali kupitia kwa Simbachawene, ilisema hali ya mafuta itarejea kama kawaida, baada ya tatizo lililosababisha kuwepo kwa uhaba wa nishati hiyo kushughulikiwa.
Naye Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alitumia kanuni za 55 (F) na 59 (B) ya kuruhusu haki za Bunge, alihoji kuhusu uundwaji wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika Makinda kutokana na kashfa za rushwa.
Kabla ya kutoa hoja hiyo ambayo hata hivyo ilikosolewa na Makinda, Mnyika alisema kwenye Bunge la bajeti iliyopita, serikali ilitoa taarifa ya utatuzi wa tatizo hilo na Novemba mwaka jana, lilipitisha maazimio ya kushughulikia gesi na petroli.
Alisema hatua hiyo ilifanyika kwa kuiruhusu Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ifuatilie suala hilo lakini kwa bahati mbaya ilivunjwa.
“Nchi haina mafuta, kamati imevunjwa, matatizo yanashindwa kushughulikiwa kwa sababu ya kukosa kamati,” alisema.
Akiikosoa hoja ya Mnyika, Makinda alisema suala hilo liliwasilishwa na Mbunge huyo kwa njia ya barua na linafanyiwa kazi.
Lakini kutokana na hoja ya Lugora, Makinda alimuita Naibu Waziri kuijibu, ambapo (Simbachawene) alisema Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, yupo jijini Dar es Salaam kufanikisha suluhu ya kudumu.
Alisema chanzo cha tatizo kilitokana na makosa ya kuruhusu meli za mafuta zinazopitia bandari ya Dar es Salaam kwenda nje ya nchi, bila kutambua kiwango cha mafuta kilichopo nchini.
Simbachawene alisema suala hilo limeshughulikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura), Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).
“Kwa hali ya sasa tatizo hili limeshughulikiwa tumeamua kuchukua mafuta ya on transit (yanayopitia nchini kwenda nje ya nchi),” alisema.
Alisema kwa upande wa Dar es Salaam tatizo hilo limekwisha kwa kuwa mafuta yameshajaa na magari makubwa yameanza kuchukua mafuta kwenda mikoani.
“Tunaamini kuwa tatizo hili halitarejea tena,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa waziri atatoa taarifa rasmi kwa kuzungumza na waandishi wa habari.
Akifunga hoja hiyo, Spika aliagiza serikali itoea taarifa rasmi siku ya Jumatatu bungeni.
EWURA YATOA TAARIFA TOFAUTI
Kwa upande wake Ewura imesema katika kukabiliana na uhaba wa mafuta, serikali imezuia lita milioni 40 za mafuta zilizokuwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi. Mafuta hayo sasa yanatarajiwa kuuzwa nchini ili kuziba pengo linalotokana na uhaba uliopo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema akiba ya lita milioni 80 zilizokusudiwa kusafirishwa kwenda nje, zilipunguzwa kwa kiwango cha asilimia 50.
Alisema serikali imeshatoa vibali kwa baadhi ya kampuni za mafuta, ili ziyauza hapa nchini ambapo mpaka sasa, kampuni tisa zimeridhia maombi hayo. Hatua hiyo itawezesha `kusambaza’ lita milioni 26.6 za petroli na diseli pamoja na mafuta ya taa yenye ujazo wa lita milioni 1.48.
Hata hivyo, wakati Simbachawene akisema mafuta hayo yameshasambazwa sokoni, Kaguo alisema utekelezaji wake haujaanza, kwa vile kampuni hizo hazijatimiza masharti ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ikiwemo kulipa kodi ya asilimia 100.
Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Mogas, Gapco, GBP, Lake Oil, Hass Petroleum, Puma, Oryxy, Engen na Camel. Hata hivyo, alisema tatizo la mafuta linatarajiwa kumalizika kwa kipindi kifupi (hakutaja) ambapo meli zilizoshindwa kupakua mafuta kutokana na kukosa nafasi ya kutia nanga, zitakakapofanya hivyo.
Alisema kutokana na ucheleweshaji, meli hizo zilisubiri kwa siku 19 bila kupakuliwa, hivyo kutumika kwa akiba ya Agosti mwaka huu, iliyokuwa kwa wafanyabiashara. Kwa mujibu wa Kaguo, kipindi hicho hapakuwa na meli iliyoleta mafuta, hivyo kusababisha uhaba wa mafuta bidhaa hiyo.
Hata hivyo, Kaguo alisema kuanzia Novemba 6 hadi 9 mwaka huu, meli zitaanza kupakuliwa mafuta na kuanza kuingia sokoni.
Akizungumzia akiba ya mafuta yaliyopo kwa sasa alisema kuwa kuna diseli lita milioni 35.8 ambayo ni matumizi ya siku 10, petrol lita milioni 16.2 ambayo ni matumizi ya siku tisa. Pia alisema yapo mafuta ya ndege yapo lita milioni 11.7 matumizi ya siku 25 na mafuta ya taa yapo lita 558,180.
WAZIRI AJITOKEZA , ATANGAZA KUFUTA LESENI ZA MAFUTA
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema uamuzi alioufikiwa ulitokana na kampuni za mafuta kufanya kazi kinyume cha taratibu huku wajumbe wa PIC wakihusika kulinda maslahi yao kibiashara.
Uamuzi huo, aliutangaza jijini Dar es Salaam jana jioni, baada ya kukutana na wafanyabiashara ya mafuta na waandishi wa habari.
Alisema sababu ya uhaba wa mafuta ni kile alichokiita kuwa ni ‘mvutano wa kizembe’ kati ya Ewura, bodi ya PIC na wafanyabiashara.
Profesa Muhongo alisema kutokana na mvutano huo, baadhi ya wafanyabiashara waliamua kupeleka mafuta nje ya nchi, wengine wakayaficha kwenye maghala kwa kisingizio kuwa bei elekezi haiwalipi faida.
Alisema kuna baadhi ya kampuni zilipewa leseni ya kuagiza mafuta, lakini biashara zao zilikuwa za mfukoni na kuisababishia serikali hasara na usumbufu.
Kutokana na hali hiyo, aliiagiza Ewura kuzifutia leseni kampuni zilizoshindwa kuingiza mafuta kwa kipindi cha miezi sita na taarifa hiyo kumfikia Jumatatu ijayo.
Profesa Muhogo alisema bodi ya PIC imevunjwa kutokana na kuwa na wafanyabiashara ambao kazi kubwa walioifanya ni kulinda biashara zao.
“Sasa bodi mpya itakayoundwa itakuwa ya kisasa na itakuwa na mjumbe mmoja mmoja kutoka idara husika na mwenyekiti atatoka wizarani,” alisema.
Alisema wajumbe wa bodi hiyo wataoka Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari (TPA), Kampuni ya kupakua na kupakia makontena bandarini (TICTS), PIC na Ewura.
Alisema bodi mpya inatarajiwa kuanza kazi ifikapo Jumanne ya wiki ijayo.
MNYIKA: POKEENI TAARIFA ZA SERIKALI KWA TAHADHARI
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amesema umma unapaswa kupokea kwa tahadhari taarifa zinazotolewa na Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake nje ya Bunge.
Alisema taarifa hizo ni zile zinazohusu masuala ya sekta ya nishati ikiwemo uhaba wa mafuta uliopo sasa, hivyo kusisitiza umuhimu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo, atoe taarifa bungeni kuhusu masuala tajwa.
Aidha, Mnyika alisema Spika Makinda anapaswa kutoa maelezo bungeni ya kuelekeza Kamati ya Kudumu ya Bunge, itakayochambua ukweli wa taarifa hizo.
“Kujirudia mara kwa mara matatizo katika sekta za nishati hususan katika biashara ya mafuta, kumechangiwa na sababu za udhaifu wa kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji wa baadhi ya viongozi na watendaji wengine…” alisema Mnyika.
Mnyika alidai kuwepo taarifa kuwa uhaba huo ni matokeo ya baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta, kuficha petroli na dizeli wakisubiri kutangazwa kwa bei mpya ya bidhaa hizo.
Kwa mujibu wa Mnyika, matatizo katika biashara ya mafuta hayahusu uhaba wa dizeli na petrol tu, bali pia kasoro katika ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.

Wanafunzi wawili wafariki kwa kugongwa na roli Mbeya.

Miili ya wanafunzi wa shule ya msingi imezu ikichukuliwa na wanausalama watoto hao walikuwa wakivuka barabara akielekea shuleni ndipo roli hilo lilipowagonga na kukimbia huku miili ya watoto hao ikiwa imetawanyika vipandevipande
Watoto hao wamegongwa katika barabara kuu itokayo Zambia kwenda dsm maeneo ya imezu inyara wilaya ya mbeya vijijini
Waanchi kwa hasira wameamua kufunga barabara hiyo wakimtaka mkuu wa mkoa mbeya aje afike eneo la tukio wamweleze kero zao za barabara hiyo kwani sasa inawamaliza wanakijiji hao kwa ajali za mara kwa mara katika eneo hilo
Habari kamili tutawaletea baadae mpaka tunaondoka eneo la tukio mkuu wa mkoa Mbeya bado hajafika eneo la tukio na habari zisizo rasmi dereva aliyewagonga watoto hao kajisalimisha katika kituo cha polisi inyala

Friday, November 2, 2012

Mnyika asisitiza Mhando, wenzake wafikishwe mahakamani.

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amesema hatua ya kufukuzwa kazi pekee kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, haitoshelezi, bali yeye na wenzake alioshirikiana nao wanapaswa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), alisema hayo kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari kupitia mtandao wa kompyuta, ikiwa ni siku moja baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, kutangaza kumwachisha kazi Mhando baada ya kukutwa na hatia ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mnyika alisema baada ya kufukuzwa kazi, serikali inatakiwa kurejea katika hotuba aliyoitoa bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya kutaka Mhando pamoja na wenzake walioshirikiana nao katika kashfa hiyo wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Pia aliitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, kueleza hatua, ambazo imezichukua kwa watendaji wengine wa shirika hilo, ambao walishirikiana na Mhando.
“…Na iwapo bodi hiyo haitachukua hatua za haraka, nitaiweka hadharani taarifa ya kamati iliyoundwa na bodi hiyo kuchambua taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kueleza hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Rais Jakaya Kikwete dhidi ya bodi yenyewe,” alisema Mnyika.
Alitaka hatua dhidi ya Mhando na wenzake waliohusika, kutogeuzwa kuwa kafara ya kuficha uzembe na udhaifu wa serikali kwa ujumla wake, kwani taarifa za utendaji wa Tanesco kuhusu mpango wa dharura wa umeme pamoja na ununuzi wa mafuta uliokuwa ukifanyika, zilikuwa zikiwasilishwa kwenye vikao vya Wizara ya Nishati na Madini na vya Baraza la Mawaziri pia.
Alisema ili ukweli wa kina ujulikane, Kambi Rasmi ya Upinzani imependekeza Bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta kwa ajili ya mitambo ya umeme.
Alitaka uchunguzi huo umshirikishe CAG katika kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi kwa malipo yaliyofanywa na kampuni ya BP, ambayo kwa sasa ni Puma, Oryx na Camel Oil,  ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme.

Mabilioni ya Uswisi:Mbowe ambana Pinda.

Serikali imezidi kuandamwa na sakata la utoroshwaji nje wa mabilioni ya fedha, baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kubanwa bungeni akitakiwa kueleza hatua zilizochukuliwa na serikal;I kurejesha nchini fedha hizo za walipa kodi. Baada ya jana kubanwa na kutakiwa kueleza uchunguzi wa fedha hizo ulikofikia, Pinda aliliambia Bunge kuwa serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa kina wa madai ya kuwepo kwa mabilioni ya fedha za kigeni zilizotoroshwa nchini na kufichwa kwenye mabenki ya ughaibuni na kwamba uchunguzi huo ukikamilika, taarifa za majina ya wahusika, hatua zitakazochukuliwa dhidi yao na mkakati wa kurejesha fedha hizo itatolewa kwa wananchi. Alitoa jibu hilo katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu lililoulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliyetaka kujua hatua na mkakati uliochukuliwa na serikali kuhusu suala ikiwamo kuwataja wahusika. Mbowe alisema fedha hizo zimehifadhiwa kwenye akaunti za viongozi waandamizi, viongozi wastaafu na wafanyabishara kinyume cha sheria na kanuni za nchi, na alisema tangu wakati wa Mkutano wa Bajeti kwa mwaka 2012/13 zilipotolewa tuhuma hizo, serikali bado imekuwa kimya kuzungumzia hatua ilizofikia katika kulishughulikia suala hilo. “Ni kweli niliahidi kutoa taarifa ya jambo hilo kwa sababu ya ukubwa wake, nilisema tutahitaji kufanya uchunguzi wa kina na hilo jambo tunalifanya na tutatoa taarifa,” alisema Pinda. Katika swali la nyongeza, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), alitaka kujua kwa nini serikali haijaamua kuomba kibali kwa Benki ya Dunia kupitia kitengo chake cha kurejesha mali (Asset Recovery Unit) ili kisaidie kurejesha fedha hizo ambazo zimefichwa sio Uswisi pekee, bali katika nchi nyingi kama vile Dubai, Jersey, Grenada, Luxemburg, Mauritius na nchi zingine kwa vile nchi hizo hazitozi kodi. Mbowe alitoa hoja hiyo akionyesha wasiwasi kuhusu uchunguzi unaofanywa kwa kuhusisha vyombo vya hapa nchi ambavyo alidai vinaweza kuwalinda wahusika. Pinda alisema: “Mheshimiwa Mbowe anaweza kulirudia suala hili mara mbili tatu, na mimi nitajibu hivi hivi kwamba uchunguzi bado unaendelea na utakapokamilika tutatoa taarifa.” “Haiwezekani suala zito kama hili lenye tuhuma nyingi likaweza kupatiwa majibu ndani ya wiki moja, nasisitiza kwamba bado tunaendelea na uchunguzi na utakapokamilika tutawaeleza hatua stahiki zilizochukuliwa,” aliongeza. Jumanne wiki hii, wakati wabunge wakichangia Azimio la Kuridhia Marekebisho ya Pili ya Mkataba wa Ushirikiano kati ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya na nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki, (ACP), Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alitaka nchi za Umoja wa Ulaya (EU), zisaidie kurejeshwa kwa mabilioni ya fedha zilizoibwa, kutoroshwa na kufichwa kwenye mabenki ya Uswisi. “EU ihakikishe mabilioni yaliyopelekwa kwenye mabenki ya Uswisi yanarejeshwa,” alisema. Alisema katika kifungu cha 29 cha ACP, kinazungumzia ushirikiano wa kikanda katika kupiga vita rushwa na mambo mengine, sasa serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba fedha zilizofichwa huko Uswisi zinarejeshwa nchini. Hoja ya kufichwa kwa mabilioni ya fedha katika benki za Uswisi kulikofanywa na baadhi ya vigogo serikalini, ilifichuliwa kwa mara ya kwanza na Chadema na katika Bunge la Bajeti ya mwaka 2012/13. Waziri Kivuli wa Fedha wa Kambi ya Upinzani, Zitto Kabwe aliitaka serikali kuwataja kwa majina vigogo waliohusika na utoroshaji wa fedha hizo Sh. bilioni 300 la sivyo, kambi ya upinzani bungeni itawataja. Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema wakati umefika kwa serikali kuliambia Taifa hatua itakazochukua kurejesha fedha hizo na nyingine zozote zilizopo ambazo imezifichwa ughaibuni. Zitto mara kwa mara amekuwa akitishia kuwa ikiwa serikali itaendelea kuficha ukweli huo na kuchukua hatua, atawataja vigogo hao kwa majina.

Thursday, November 1, 2012

Polisi washusha bendera za Uamsho Z’bar

BAADA ya kuchoshwa na vitendo vya kihuni vinavyofanywa visiwani hapa, Serikali imeamua kusafisha vigenge hivyo, ikiwa ni pamoja na kushusha bendera za Jumuiya ya Uamsho zilizokuwa zikipepea katika maeneo mbalimbali mitaani mjini hapa. Kazi hiyo inafanywa na Jeshi la Polisi ambalo limethibitisha kusaka vikundi hivyo vya kihuni ambavyo vimekuwa vikijipachika majina mbalimbali kwa kutumia mwavuli wa Jumuiya hiyo kufanya fujo. Akizungumza kwa simu jana, Kamishna wa Polisi, Musa Ali Musa, alisema polisi wamekuwa wakifanya msako dhidi ya vigenge vya vijana wanaofanya uhalifu na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi. “Jeshi la Polisi linachokifanya ni kutafuta vigenge vinavyofanya uhuni na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria … tumeanza kuwabaini baada ya kutumia teknolojia kupitia video,” alisema Musa. Alisema baadhi ya vijana wameanza kukamatwa baada ya picha zao kuonekana kwenye maandamano ya Jumuiya ya Uamsho wakiwa na mapanga huku wakitoa kauli za ‘Chinja! Chinja’! “Polisi haifanyi kazi kwa kukiuka misingi ya haki za binadamu … tunawafuata wahusika wa fujo baada ya kuwatambua,” alisema Kamishna Musa. Taarifa zilizopo zilisema zaidi ya bendera 50 ziliteremshwa katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Bububu, Mboriborini na Daraja bovu. Aidha, ulinzi mkali na msako vinaendelea katika maeneo kadhaa ya mji ikiwa ni pamoja na Bububu ambako aliuawa askari Said Abrahman kwa kushambuliwa na watu wasiojulikana wakamjeruhi na kusababisha mauti yake. Hivi karibuni, Jeshi la Polisi lilionesha picha za baadhi ya vijana wakiwa mstari wa mbele kwenye maandamano ya Jumuiya ya Uamsho, huku wakiwa na mapanga na Polisi kuomba msaada kwa wanaowajua kutoa taarifa ili kufikishwa kunakohusika. Akihutubia Baraza la Iddi mjini hapa, Rais Ali Mohamed Sheni alisema uvumilivu wa Serikali sasa umefika kikomo na kuongeza kwamba vyombo vya Dola vitachukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuvunja sheria za nchi huku akisisitiza hakuna aliye juu ya sheria. Jumuiya ya Uamsho imeingia katika matatizo na Serikali baada ya wafuasi wake wakiongozwa na Shekhe Farid Hadi Ahmed, kutokana na kufanya maandamano na vurugu.

MBOWE KUIPONGEZA SERIKALI YA JK

KIONGOZI wa Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ameisifu na ameipongeza Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa na yenye mafanikio ya kujenga miundombinu nchini. Aidha, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai kupitia Chadema, amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Kikwete katika ujenzi wa nchi, akisisitiza kuwa “huyu ndiye kiongozi wetu, ndiye mkuu wetu na wa nchi yetu.” Mbowe alitoa sifa na pongezi hizo kwa Rais Kikwete wakati wa sherehe ya uwekaji jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya Kwasadallah- Masama katika Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro uliofanywa na Rais Kikwete kwenye siku ya nne na ya mwisho ya ziara yake mkoani Kilimanjaro kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo. Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 12.5 iliahidiwa na Rais Kikwete mwenyewe baada ya kusikia kilio cha miaka mingi cha wakazi wa Masama ambao wamekuwa wanaiomba Serikali kuwajengea barabara kama ilivyo kwa wenzao wa Machame katika wilaya hiyo hiyo ya Hai. Barabara hiyo inayogharimu kiasi cha Sh bilioni 5.3, ni moja ya barabara nne zinazojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Kilimanjaro kwa gharama ya Sh bilioni 32.55. Akizungumza wakati alipopewa nafasi kuwasalimia wananchi kwenye sherehe hiyo ya kuweka jiwe la msingi, Mbowe alisema: “Tunakushukuru sana wewe binafsi Mheshimiwa Rais, naishukuru sana Serikali yako, namshukuru sana Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Magufuli (John Magufuli) kwa ujenzi mkubwa sana wa barabara za nchi yetu. Haijapata kutokea katika historia ya nchi yetu. Mmefanya kazi kubwa sana katika kuiunganisha nchi yetu kwa mtandao mkubwa wa barabara,” alisema Mbowe. Kuhusu ujenzi wa Barabara ya Kwasadallah-Masama, Mbowe alimwambia Rais: “Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ahadi yako ya kututengenezea barabara hii kwa sababu huko juu milimani kuna watu wengi ambao wanazalisha mazao ya chakula kwa wingi.” Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Dk Magufuli alielekeza watendaji wa taasisi zilizoko chini yake kumchukulia hatua mkandarasi wa barabara hiyo, Kampuni ya Atlantic Marketing Limited, ambayo alitakiwa kumaliza barabara hiyo miaka minne iliyopita, lakini mpaka sasa anasuasua pamoja na kwamba amelipwa fedha yote ya ujenzi. Naye Rais Kikwete alisema ni dhamira ya Serikali yake kuwa ifikapo mwaka 2015, Tanzania iwe na mnyororo mmoja mkubwa wa barabara za lami na ndiyo maana kazi inaendelea kuchapwa katika sehemu mbalimbali nchini kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwa barabara za lami. Alisema kuwa sera ya Serikali yake ni kuunganisha mikoa yote kwa lami, kujenga barabara zote kuu kiuchumi kwa lami na pia kujenga madaraja yote makubwa 12 nchini. Rais pia alisema kazi hiyo ya kujenga barabara kwa ajili ya wananchi inafanyika bila kujali tofauti za kisiasa za maeneo ambako barabara zinajengwa. “Nyinyi hapa mlimchagua Mbowe. Hii ndiyo demokrasia na wala hatuna ugomvi na chaguo lenu. Lakini Mbowe huyu hana Serikali, sisi ndiyo wenye Serikali na ni wajibu wetu kuwajengea Watanzania wote bila ubaguzi barabara za lami. Kumchagua Mbowe ilikuwa hiari yenu hata kama sisi katika CCM tulipenda Mbunge wa Hai awe wa chama chetu,” alisema Rais Kikwete. Rais Kikwete alimaliza ziara yake mkoani Kilimanjaro na amekwenda Dodoma kwa ziara ya kikazi.