HABARI MOTO MOTO ...

Tuesday, November 27, 2012

Radi yaua watatu wakisali chini ya mti

Watu watatu wamekufa papo hapo wawili wa familia moja na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na radi wakati wakifanya ibada chini ya mti katika kitongoji cha Mtakuja, kijiji cha Kivingo, kata ya Longuza, wilayani hapa.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 10:30 jioni huku kukiwa na upepo mkali uliombatana na manyunyu ya mvua.

Afisa Tarafa ya Umba, Mpemba Gabriel, aliwataja waliokufa kwa kupigwa na radi hiyo kuwa ni Esther Moleto, Salome Sengasu na ndugu yake Naiyo Sengasu.

Gabriel alisema kuwa majeruhi wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Mnazi kwa matibabu.

“Walikuwa chini ya mti wakiendelea na ibada ghafla hali ya hewa ilibadilika na kuibuka upepo mkali ulioambatana na mvua,” alisema Gabriel.

Naye Afisa Tarafa ya Mlalo, Dunstan Mudu, alisema kuwa kabla ya tukio hilo kulikuwa na ngurumo za radi zilizoambatana na upepo mkali.

Mudu alisema hali hiyo iliwatisha wakazi wa maeneo hayo na kulazimika kuacha shughuli zao kisha wakajifungia ndani ya nyumba zao.

Kufuatia tukio hilo, viongozi wa serikali wa ngazi za kata, tarafa hadi wilaya ya Lushoto, wamewashauri wananchi kutokaa karibu na miti wakati mvua zinaponyesha.

Alisema wilaya ya Lushoto imezungukwa na milima na misitu ya asili ambayo ni kichocheo kikubwa cha radi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Kata ya Longuza, Sadick Singano, alisema wilaya ya Lushoto imezungukwa na milima mingi huku makazi ya watu yakiwa chini.

Sungano alisema kuwa kwa kawaida radi hufuata miti na kuwataka wanaolima mabondeni kuwa makini kwani lolote linaweza kutokea.

No comments:

Post a Comment