HABARI MOTO MOTO ...
Tuesday, November 6, 2012
Askofu Balina afariki.
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Aloysius Balina, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Antony Makunde, imesema kuwa Askofu Balina amefariki jana mchana, kutokana na maradhi ya saratani ya ini kwa muda mrefu.
Padre Makunde alisema kuwa, mapema mwaka huu, Askofu Balina alipelekwa Ujerumani kwa matibabu, na akarejea nchini akiwa mwenye afya njema.
Hata hivyo, miezi michache alianza tena kusumbuliwa na ugonjwa huo, na afya yake ilizidi kudorora ambapo mwezi uliopita, alilazwa katika Hospitali ya Bugando kabla ya kufikwa na umauti jana.
Askofu Balina alizaliwa Juni 21,1945, Ntuzu, Bariadi mkoani Shinyanga.
Baada ya kuhitimu masomo yake mbalimbali, alipewa daraja la upadri Mei 26, 1971.
Kutokana na utumishi wake mwema, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua kuwa askofu wa Jimbo la Geita mwaka 1985. Septemba 1997, aliteuliwa kuwa askofu wa Jimbo la Shinyanga ambako alilitumikia hadi jana alipoitwa na Mungu.
Wakati wa uhai wake, Askofu Balina alishikilia nafasi kadhaa ndani ya Baraza la Maaskofu ambako kwa miaka mingi alikuwa mwenyekiti wa idara ya afya ya baraza hilo, na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Bugando.
Askofu Balina ni mmoja wa maaskofu wachache wa Kikatoliki ambaye alitazama maisha ya waamini wake na watu wote wa majimbo ya Geita na Shinyanga, katika mahitaji yote ya kiroho na kimwili.
Aidha, ni mmoja wa viongozi wa dini aliyesimamia kikamilifu kuinua Hospitali ya Bugando na hasa juhudi zake zilizosukuma kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Afya Bugando.
Kadhalika, alifanya kazi kubwa akishirikiana na maaskofu wenzake, kuhakikisha kuwa kinaanzishwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine, na hatimaye kufikia mafanikio makubwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment