Akizungumza kwenye uwanja wa Azam Complex
mara baada ya mchezo kati ya Azam na Coastal Union juzi, Brandts alisema
licha ya Yanga kuwa kwenye kasi kwa sasa, watakuwa na kazi ngumu mbele
ya timu hiyo.
"Nawafahamu Azam tangu kwenye mashindano
ya Kombe la Kagame, na leo nimepata nafasi ya kuwaona tena," alisema
Brandts na kueleza zaidi kuwa "ni timu nzuri na inayocheza soka la
kisasa kwa sababu wachezaji wake wana stamina na wanacheza soka la
nguvu.
"Kwa kweli tutakuwa na kazi ngumu kwenye mchezo wetu wa Jumapili (kesho)."
Aidha, alisema kuwa atatumia mapungufu
aliyoyaona kwenye mchezo wa timu hiyo dhidi ya Coastal Union kuhakikisha
kikosi chake kinapata matokeo mazuri kwenye mchezo wa kesho.
Alisema katika kikosi hicho cha Azam, ambayo juzi iliifunga Coastal 4-1, anamuhofia mshambuliaji John Bocco.
Aliema mchezaji huyo anajua kufanya kazi yake na kwamba kwake itakuwa furaha kama atakosekana kwenye mchezo huo.
Hata hivyo, habari ambazo Nipashe
imezipata na kuthibitishwa na msemaji wa Azam, Jaffar Iddi, Bocco
atakuwepo kikosini kesho baada ya kupona majeraha aliyoyapata kwenye
mchezo wa kichapo cha magoli 3-1 dhidi ya Simba wiki iliyopita.
"Bocco anaendelea vizuri na hakuna shaka
Jumapili (kesho) atakuwepo uwanjani kutegemea na kocha atakavyoamua...
ila yuko vizuri baada ya kupona majeraha yake," alisema Iddi.
Kocha huyo wa Yanga alisema wachezaji wake
kwa sasa wapo katika hali nzuri kimwili na kiakili; hasa baada ya
kuibuka na ushindi mfululizo kwenye ligi kuu wakifuta machungu ya kuanza
vibaya katika michezo minne ya mwanzoni mwa msimu.
Azam itaikaribisha Yanga kesho kwenye
Uwanja Taifa, ukiwa ni mchezo wao wa kwanza wa timu hizo tangu mabingwa
wa Afrika Mashariki na Kati hao waifunge timu hiyo ya wauza vyakula 2-0
kwenye fainali ya Kombe la Kagame Julai.

No comments:
Post a Comment