Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameingilia kati sakata la muuguzi afya (nesi) wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita la kuwanyofolea chupa za maji ya dawa (drip) watoto saba waliolazwa hospitalini hapo.
Kutokana na tukio hilo ambalo lingeweza
kusababisha vifo, Waziri Magufuli alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya
(OCD) wa Chato kumkamata na kumfikisha mahakamani nesi huyo (jina
tunalihifadhi) kwa kitendo hicho.
Inadaiwa kuwa nesi huyo alifikia maamuzi
ya kuwaadhibu watoto kwa kuwakatia dawa baada wazazi wao kukataa kufanya
usafi kwenye vyoo vya hospitali hiyo.
Tukio hilo ambalo limetokea jana majira ya
asubuhi liliwalazimisha wazazi wa watoto hao kufanya mawasiliano na
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya ndugu wa watoto hao
walipiga simu kwa Katibu wa Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa
Ujenzi aliyewasili hopitalini hapo akifuatana na kamati ya ulinzi na
usalama ya wilaya hiyo.
Akizungumza na wagonjwa, madaktari na
wauguzi (manesi) na wahudumu wa afya, Dk. Magufuli alisema kitendo
kilichofanywa na nesi huyo hakistahili kufumbiwa macho kwa kuwa
kililenga kupoteza uhai wa wagonjwa waliokuwa wanaendelea kutumia dawa
kutokana na maelekezo waliyopewa na madaktari.
Alisema kutokana na malalamiko mengi ya
wagonjwa kuhusiana na huduma za afya zinazotolewa hospitalini hapo, kuna
haja ya kutafuta mwarobaini wa kutibu vitendo vya ukiukwaji wa sheria
vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Idara ya Afya ambao wamekuwa
wakifanya kazi kwa mazoea.
Kufuatia hali hiyo, Magufuli alimwagiza
OCD wa Chato, Leonard Nyaoga, kuhakikisha Jeshi lake linamsaka na
kumfikisha mahakamani nesi huyo kwa tuhuma za kutaka kusababisha vifo
vya watu saba kinyume cha sheria.
Vilevile amemwagiza Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya hiyo, Shaban Ntarambe, kumsimamisha kazi mara moja
wakati taratibu za kisheria zikiwa zinaendelea na kwamba hatakiwi
kuonekana akitoa huduma kwenye hospitali hiyo kwa kuwa kitendo chake
kimethibitisha kuwa hana sifa za kuwa muuguzi.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo,
ambaye aliongozana na Waziri Magufuli, alisema serikali inalishughulikia
tukio hilo mpaka hapo sheria itakapochukua mkondo wake kwa kuwa kitendo
kilichofanywa na muuguzi huyo siyo cha kiuungwana.
Mpongolo aliwataka wagonjwa wanaofika
hospitalini hapo kupata matibabu kutoa ushirikiano kwa viongozi wa
hospitali yanapotokea matukio ambayo yanaweza kuhatarisha maisha
kutokana na utendaji kazi mbovu wa baadhi ya watumishi.
Pia, aliahidi kuunda kamati maalum
itakayochunguza huduma za afya zinazotolewa katika hospitali hiyo
kufuatia malalamiko mengi ya wananchi.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Pius
Buchukundi, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba ofisi yake
imekwisha kuchukua hatua za kuhakikisha mtumishi huyo anawajibishwa
kulingana na kosa alilotenda.
Dk. Buchukundi alisema kitendo cha watoto
saba kuondolewa maji yenye dawa hakikufanywa kwa maelekezo ya uongozi wa
hospitali hiyo bali ni maamuzi binafsi ya mtumishi huyo kwa matakwa
yake binafsi.
Aliwahakikishia wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali hiyo kuwa tukio kama hilo halitajitokeza tena.
Aliwataja watoto ambao walinyofolewa drip
kuwa ni Edward Robert (4), mkazi wa kijiji cha Nyamirembe; Kashinje
Lukanya (12), mkazi wa Busaka; Iren Nasib (3), mkazi wa Bwanga; Naomi
Tumain (5), mkazi wa Kachwamba; Yunis William (3), mkazi wa Kasala;
Asteria Siajali (2), mkazi wa Kahumo na Alphonce Makolobelo.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, Ester
Misungwi, Sindikwi Mkubulo na William Masai, waliipongeza hatua ya
Waziri Magufuli kuhakikisha mhusika wa tukio hilo anakamatwa na
kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili ili liwe fundisho kwa
watumishi wengine wenye tabia kama hizo.
Juhudi za NIPASHE kumpata muuguzi huyo ili kuzungumzia tukio hilo la aina yake katika fani ya utabibu hazikuzaa matunda jana.

No comments:
Post a Comment