HABARI MOTO MOTO ...

Thursday, November 1, 2012

MBOWE KUIPONGEZA SERIKALI YA JK

KIONGOZI wa Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ameisifu na ameipongeza Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa na yenye mafanikio ya kujenga miundombinu nchini. Aidha, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai kupitia Chadema, amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Kikwete katika ujenzi wa nchi, akisisitiza kuwa “huyu ndiye kiongozi wetu, ndiye mkuu wetu na wa nchi yetu.” Mbowe alitoa sifa na pongezi hizo kwa Rais Kikwete wakati wa sherehe ya uwekaji jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya Kwasadallah- Masama katika Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro uliofanywa na Rais Kikwete kwenye siku ya nne na ya mwisho ya ziara yake mkoani Kilimanjaro kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo. Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 12.5 iliahidiwa na Rais Kikwete mwenyewe baada ya kusikia kilio cha miaka mingi cha wakazi wa Masama ambao wamekuwa wanaiomba Serikali kuwajengea barabara kama ilivyo kwa wenzao wa Machame katika wilaya hiyo hiyo ya Hai. Barabara hiyo inayogharimu kiasi cha Sh bilioni 5.3, ni moja ya barabara nne zinazojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Kilimanjaro kwa gharama ya Sh bilioni 32.55. Akizungumza wakati alipopewa nafasi kuwasalimia wananchi kwenye sherehe hiyo ya kuweka jiwe la msingi, Mbowe alisema: “Tunakushukuru sana wewe binafsi Mheshimiwa Rais, naishukuru sana Serikali yako, namshukuru sana Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Magufuli (John Magufuli) kwa ujenzi mkubwa sana wa barabara za nchi yetu. Haijapata kutokea katika historia ya nchi yetu. Mmefanya kazi kubwa sana katika kuiunganisha nchi yetu kwa mtandao mkubwa wa barabara,” alisema Mbowe. Kuhusu ujenzi wa Barabara ya Kwasadallah-Masama, Mbowe alimwambia Rais: “Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ahadi yako ya kututengenezea barabara hii kwa sababu huko juu milimani kuna watu wengi ambao wanazalisha mazao ya chakula kwa wingi.” Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Dk Magufuli alielekeza watendaji wa taasisi zilizoko chini yake kumchukulia hatua mkandarasi wa barabara hiyo, Kampuni ya Atlantic Marketing Limited, ambayo alitakiwa kumaliza barabara hiyo miaka minne iliyopita, lakini mpaka sasa anasuasua pamoja na kwamba amelipwa fedha yote ya ujenzi. Naye Rais Kikwete alisema ni dhamira ya Serikali yake kuwa ifikapo mwaka 2015, Tanzania iwe na mnyororo mmoja mkubwa wa barabara za lami na ndiyo maana kazi inaendelea kuchapwa katika sehemu mbalimbali nchini kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwa barabara za lami. Alisema kuwa sera ya Serikali yake ni kuunganisha mikoa yote kwa lami, kujenga barabara zote kuu kiuchumi kwa lami na pia kujenga madaraja yote makubwa 12 nchini. Rais pia alisema kazi hiyo ya kujenga barabara kwa ajili ya wananchi inafanyika bila kujali tofauti za kisiasa za maeneo ambako barabara zinajengwa. “Nyinyi hapa mlimchagua Mbowe. Hii ndiyo demokrasia na wala hatuna ugomvi na chaguo lenu. Lakini Mbowe huyu hana Serikali, sisi ndiyo wenye Serikali na ni wajibu wetu kuwajengea Watanzania wote bila ubaguzi barabara za lami. Kumchagua Mbowe ilikuwa hiari yenu hata kama sisi katika CCM tulipenda Mbunge wa Hai awe wa chama chetu,” alisema Rais Kikwete. Rais Kikwete alimaliza ziara yake mkoani Kilimanjaro na amekwenda Dodoma kwa ziara ya kikazi.

No comments:

Post a Comment