KWA mara nyingine tena, jiji la Mwanza limegeuka kuwa uwanja wa
mapambano baada ya kuibuka mapigano makali baina ya mgambo na
wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga.
Katika mapigano hayo yaliyotokea jana majira ya saa tano asubuhi,
polisi na mgambo hao walilazimika kutumia risasi za moto kujihami na
hivyo kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyepigwa risasi na mgambo.
Mbali na kuuawa kwa mtu huyo, pia wengine wawili walijeruhiwa vibaya
kwa risasi katika mapambano hayo yaliyofanyika kwenye makutano ya
barabara ya Pamba, Miti Mirefu na stendi ya zamani ya Tanganyika iliyoko
katikati ya jiji.
Chanzo cha vurugu hizo kinaelezwa kuwa ni mgambo wa jiji waliokuwa
kwenye operesheni ya kuwaondoa Machinga hao kwenye maeneo yasiyoruhusiwa
kisheria kufanya biashara.
Ilielezwa kuwa mgambo hao walifika maeneo hayo ya barabara ya Pamba
kisha kuanza kukamata bidhaa za Machinga na kuondoka nazo bila wahusika
kuwakamata.
Mashuhuda walidai kuwa tukio hilo liliwapandishia hasira Machinga hao
kisha kuanza kuwashambulia kwa mawe askari hao wa jiji ambao baadaye
walilazimika kujihami kwa kufyatua risasi za moto zilizogharimu maisha
ya mmoja wa Machinga hao maarugu kama ‘Chapombe’.
Msako huo ulidaiwa kufanywa kimya kimya na mgambo hao badala ya kutoa
tangazo kwa wahusika kuondoka maeneo hayo kama sheria inavyosema.
“Mimi nimeshuhudia kabisa mgambo wa jiji wakichukua bidhaa za
Machinga, baadaye Machinga nao wakakasirika na kuanza kuwarushia mawe,
ndipo mgambo wakaanza kufyatua risasi wakiwalenga watu,” alisema
shuhuda.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola, alithibitisha
kuuawa kwa risasi mtu mmoja katika mapambano na kumtaja marehemu kuwa
alikuwa mpiga debe.
“Leo zilizuka vurugu kubwa kati ya Machinga na mgambo wa jiji. Vurugu
hizi zilitokea baada ya Machinga kumkimbilia na kumkwida mgambo
shingoni kisha kumtolea sime.
“Baada ya kuona hivyo, mgambo waliokuwa kwenye operesheni
walilazimika kujihami kwa kufyatua risasi hewani, lakini bahati mbaya
ilimpata mpiga debe na kufa papo hapo na wengine wawili walijeruhiwa na
wamelazwa Hospitali ya Bugando,” alisema Matola.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, alieleza
kusikitishwa na vurugu hizo na kusema mgambo hao walikuwa kazini kama
walivyopangiwa katika utaratibu wa kawaida.
Kwa mujibu wa Kabwe, utaratibu na sheria za jiji la Mwanza ni
kuwaondoa Machinga katikati ya jiji na kwamba operesheni ya mgambo ya
kuwaondoa Machinga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria bado
inaendelea.
Hili ni tukio la tatu kwa pande hizo kuzua vurugu tangu kumalizika
Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 na katika matukio yote watu walipigwa na kuuawa
kwa risasi, jambo linalolalamikiwa na wananchi.
Polisi na ‘majambazi’
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi mkoani hapa, limewaua watu
wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi katika tukio la kurushiana risasi
usiku wa kuamkia jana katika Big Bite Kilimahewa Wilaya ya Ilemela.
Kamanda Matola aliwaambia waandishi wa habari kwamba tukio hilo
lilitokea majira ya saa 5 usiku wa Novemba 14, mwaka huu, ambapo katika
majibizano ya risasi na watuhumiwa hao watano, watatu walifanikiwa
kukimbia huku polisi wakiwapokonya bunduki aina ya SMG na risasi 43.
Hili ni tukio la kwanza la polisi kurushiana risasi na majambazi
tangu mauaji ya aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Liberatus
Barlow, yaliyofanyika hivi karibuni.
Machinga mwingine amejeruhiwa kwenye mkono wa kushoto katika kiwiko, naye dereva wa magari ya biashara za kusafirisha mizigo wa gari aina ya Kenta, magari ambayo hupaki katika eneo hilo amejeruhiwa upande wa kushoto kichwani na kukimbizwa hospitali ya rufaa Bugando kwa matibabu.
Mkuu wa polisi (OCD) wa wilaya ya Nyamagana Ally Kitumbu. akizungumza na wafanyabiashara hao wadogo (wamachinga) kuendelea na kazi kwa kufuata sheria wakati jeshi hilo likifanya uchunguzi wa tukio hilo.
Mmoja wa viongozi wa akiwatuliza wamachinga wenzake kupata kumsikiliza mkuu wa polisi (OCD) wa wilaya ya Nyamagana Ally Kitumbu. .




No comments:
Post a Comment