Jeshi la Polisi la Mkoa wa Pwani,
linamshikilia Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, Rehema Gogo
(34) kwa tuhuma za kuiba kichanga cha siku moja.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mganga Mkuu wa Hospitali
hiyo, Dk. Phransisco Mwamisi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Ni kweli kichanga hicho kiliibwa na muuguzi wa pale hospitali siku ya
Novemba 10, mwaka huu, majira ya saa tano asubuhi,” alisema Mwamisi.
Alisema muuguzi huyo kwa sasa ameshikiliwa na Jeshi la Polisi tangu siku ya tukio.
Jeshi la Polisi Wilaya hiyo lilithibitisha kutokea wizi wa kichanga hicho.
Kwa mujibu wa jeshi hilo, mtuhumiwa huyo, ambaye alikuwa likizo, alikodi
gari na kwenda hospitalini hapo na kuingia katika wodi ya wazazi.
“Aliingia wodini humo na kuchukuwa kichanga na kumfunika kwenye hijabu
yake. Mama wa mtoto huyo alikuwa ametoka nje kwenda kupiga simu kwao,
kwani alijifungua usiku na aliporudi hakumkuta mtoto wake,” alisema
mmoja wa maofisa waandamizi wa jeshi hilo wilayani humo.
No comments:
Post a Comment