Mwalimu wa Shule ya Msingi
Kwamwachalima iliyopo katika kijiji cha Kwamwachalima, kata ya Komkonga,
Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Nangoma Suhalungi Nangoma (23),
anatuhumiwa kumuua kwa kisu mwanafunzi wake na kumjeruhi mwingine.
Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, polisi wanamtafuta mtuhumiwa huyo ili afikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Mwalimu huyo anadaiwa kumuua mwanafuzi wa darasa la tatu katika shule hiyo.
Kadhalika, mwalimu huyo anakabiliwa na tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi
wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kisaza iliyopo katika kata
hiyo.
Habari kutoka katika eneo la tukio ambazo zimethibitishwa na Mkuu wa
Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, zilieleza kwamba tukio hilo
lilitokea Novemba 23, mwaka huu saa 9:00 usiku baada ya muuaji kuwavamia
watoto hao chumbani kwao na kuwachoma kisu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huku akiwa na huzuni shuleni
hapo, baba wa marehemu, Ijumaa Mjaliwa, alimtaja binti yake aliyepoteza
maisha kuwa ni Farihia Mjaliwa (9) na aliyejeruhiwa ni Mohamed Mjaliwa
(16).
Mohamed ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Sekondari ya Kisaza.
“Aliyemuua mwanangu na kumjeruhi kijana wangu ni Mwalimu mwenzangu
ambaye tunafundisha wote hapa shuleni. Alimchoma kisu kifuani eneo la
moyoni. Sina ugomvi naye na tunakaa nyumba moja ila usiku mimi sikulala
hapa,” alisema Mjaliwa na kuongeza:
“Yeye alikuwa na kesi ya kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili,
hivyo alikuwa nje kwa dhamana, jana walimu wote tulifanya kikao cha
kujadili namna ya kumuwekea dhamana mahakamani, maana kesho yake
kulikuwa na taarifa kwamba angepelekwa mahakamani kujibu mashitaka hayo,
ila yeye katika mkutano huo hakuwapo.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo, Ali Hatibu, alisema
walimhoji majeruhi huyo kabla hajapoteza fahamu na kumtaja mwalimu huyo
kwamba ndiye aliyewachoma kisu pamoja na marehemu.
“Tuliingia chumbani kwa watoto na kukuta damu lakini pia binti huyu
ambaye sasa ni marehemu, tulimkuta akiwa tayari amekufa huku akiwa
ameshika kisu. Amechomwa kwenye moyo akakiacha mwilini, binti
akakichomoa na kupoteza maisha muda huo huo, yaani tukio hili
linasikitisha sana maana mtoto hakujua kinachotokea,” alisema Hatibu.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Eva Msenga, alisema siku ya tukio majira ya
mchana, alimhoji mwalimu huyo kutokana na mwenendo wake kuonekana si wa
kawaida, na kumjibu kwamba amechanganyikiwa kutokana na suala
linalomkabili la kufikishwa mahakamani, hivyo alimtaka afike ofisini
kwake ajieleze.
“Mimi nilikuwa na watoto hawa usiku hadi saa tatu, wakijisomea
nikawaambia wakalale kwa kuwa muda wa kupumzika ulikuwa umefika,
wakaenda kulala baadaye usiku wa manane ndipo mtuhumiwa akabisha hodi na
kufunguliwa kisha akaanza kufanya ukatili huo wa kutisha,” alidai
Msenga.
Akizungumza wakati akiwafariji familia iliyokumbwa na mkasa huo shuleni
hapo, Mkuu wa wilaya hiyo Rweyemamu, aliwataka wananchi kuwa na subira
katika kipindi hiki kigumu, akisema kwamba serikali imeanza kumchukulia
hatua mwalimu huyo kwa kufunga akaunti yake benki.
Rweyemamu ameomba vyombo vya habari kusaidia kumfichua mtuhumiwa huyo
ambaye ni mwenyeji wa mikoa ya Kusini ili sheria ifuate mkondo wake.
“Atakamatwa tu, tutafanya kila namna kwa kuchukua hatua aina zote
kuhakikisha kwamba mwalimu huyu anakamatwa ili apambane na mkono wa
sheria,” alisema Rweyemamu ambaye alifuatana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya
(OCD), Aziz Kimata.
Mwili wa marehemu huyo ulisafirishwa kupelekwa Chalinze wilayani Bagamoyo na mazishi yalitarajiwa kufanyika jana eneo hilo.
No comments:
Post a Comment