HABARI MOTO MOTO ...

Friday, November 16, 2012

Operesheni ya Magufuli magari ya serikali leo

Kikosi cha Usalama Barabarani, kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, leo kinafanya operesheni ya nchi zima ya kukagua magari ya umma yanayotumia namba za kiraia badala ya namba stahiki zinazotakiwa kutumika katika magari ya umma. Akizunguzna na NIPASHE ofisini kwake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alisema wanafanya operesheni hiyo kufuatia agizo alilolitoa Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli la kutaka magari yote ya umma yenye namba za kiraia, yarejeshwe kwenye namba stahiki za magari hayo. Kamanda Mpinga alisema baadhi ya vitu watakavyokuwa wanaangalia katika operesheni hiyo ni sehemu ya kioo cha gari pamoja na stika ya bima. “Inawezekana wengine wakaghushi namba, lakini tumejipanga, kuna vitu tutakuwa tunaangalia, kwa hiyo tutazibaini tu,” alisema. Dk. Magufuli aliwaagiza wale wote wanaotumia namba za kiraia katika magari ya umma, wawe wameyasajili katika namba stahiki na mwisho wa kutekeleza agizo hilo ilikuwa ni jana. Lengo la Dk. Magufuli kuanzisha operesheni hiyo ni kudhibiti matumizi mabaya ya magari ya umma yanayotumia namba za kiraia katika shughuli binafsi na hivyo kuisababishia serikali hasara. Dk. Magufuli alisema operesheni hiyo itahusisha magari yote ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala wa Serikali, Mashirika ya Umma na taasisi nyingine za umma na kwamba watawachukulia hatua walionunua magari hayo, lakini bado wanatumia namba zinazoonyesha kuwa ni milki ya serikali.

No comments:

Post a Comment