Mbunge CCM ataka `kuishughulikia` Serikali
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene
Mazingira Wakati Naibu Waziri wa Nishati
na Madini, George Simbachawene, akiliambia Bunge, mafuta yameanza
kusambazwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imesema
utekelezaji wake bado haujaanza.
wakati hali ikiwa hivyo, Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ametangaza kufutwa leseni za
biashara ya mafuta kwa kampuni zilizokiuka taratibu.
Pia ameivunja bodi ya kampuni ya uingizaji
mafuta nchini (PIC) kwa madai kuwa inaundwa na wajumbe walio
wafanyabiashara ya mafuta wasiokuwa na uwezo katika sekta hiyo.
Lakini hali ilivyo sasa, mikoa kadhaa
kadhaa imejikuta katika kadhia hiyo, hali iliyomsababisha Mbunge wa
Mwibara (CCM), Alphaxard Lugora kulitaka Bunge lisitishe shughuli zake
jana na kulijadili tatizo hilo.
Hatua ya Lugora imeilazimisha serikali
kutoa tamko la awali bungeni, kupitia kwa Simbachawene, ikisema
limeshaanza kushughulikiwa na hali imeanza kurejea kuwa ya kawaida.
Wakati Bunge likielezwa hivyo jana, Meneja
Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, aliwaambia waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam kuwa, hali ya upatikanaji mafuta bado ni ngumu.
Katika tukio la bungeni, baada ya Spika
Anne Makinda kumaliza matangazo jana asubuhi, Lugora alitumia kanuni ya
47 kutaka shughuli za Bunge zisitishwe, badala yake kujadiliwa hali ya
dharura ya uhaba wa mafuta nchini.
Hoja hiyo iliungwa na wabunge wengi
kupitia mfumo wa kusimama, ambapo walikuwemo wa CCM na wanaotokana na
vyama tofauti vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Akiwasilisha hoja hiyo, Lugora alisema upatikanaji wa nishati hiyo hususani dizeli na petroli ni mbaya kuliko maelezo.
Alisema sasa hivi imefikia hatua ambapo
mteja akienda kununua bidhaa hiyo kwenye vituo vya mafuta, anapimiwa kwa
`vibaba’. “Mimi mwenyewe niliambiwa nipewe lita 10 ili wengine waweze
kupata,” alisema.
Alisema hali kama hiyo inaweza kuwatokea
watu tofauti wakiwemo wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma ya gari
maalum la kusafirishia wenye matatizo ya afya.
Lugora alisema kutokana na `unyeti’ wa
jambo hilo, kuna wasiwasi wa kukwepo kwa hujuma kutoka kwa kampuni
kubwa, ionekane Sheria ya Ununuzi wa Jumla (bulk procurement)
imeshindikana hivyo kurejesha ununuzi wa rejareja.
Lugora aliomba wabunge wamuunge mkono hoja
yake hiyo, ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo, ambapo idadi kubwa ya
wabunge ilifanya hivyo.
Hata hivyo, serikali kupitia kwa
Simbachawene, ilisema hali ya mafuta itarejea kama kawaida, baada ya
tatizo lililosababisha kuwepo kwa uhaba wa nishati hiyo kushughulikiwa.
Naye Mbunge wa Ubungo (Chadema), John
Mnyika, alitumia kanuni za 55 (F) na 59 (B) ya kuruhusu haki za Bunge,
alihoji kuhusu uundwaji wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na
Spika Makinda kutokana na kashfa za rushwa.
Kabla ya kutoa hoja hiyo ambayo hata hivyo
ilikosolewa na Makinda, Mnyika alisema kwenye Bunge la bajeti
iliyopita, serikali ilitoa taarifa ya utatuzi wa tatizo hilo na Novemba
mwaka jana, lilipitisha maazimio ya kushughulikia gesi na petroli.
Alisema hatua hiyo ilifanyika kwa
kuiruhusu Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ifuatilie suala hilo
lakini kwa bahati mbaya ilivunjwa.
“Nchi haina mafuta, kamati imevunjwa, matatizo yanashindwa kushughulikiwa kwa sababu ya kukosa kamati,” alisema.
Akiikosoa hoja ya Mnyika, Makinda alisema suala hilo liliwasilishwa na Mbunge huyo kwa njia ya barua na linafanyiwa kazi.
Lakini kutokana na hoja ya Lugora, Makinda
alimuita Naibu Waziri kuijibu, ambapo (Simbachawene) alisema Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, yupo jijini Dar es Salaam
kufanikisha suluhu ya kudumu.
Alisema chanzo cha tatizo kilitokana na
makosa ya kuruhusu meli za mafuta zinazopitia bandari ya Dar es Salaam
kwenda nje ya nchi, bila kutambua kiwango cha mafuta kilichopo nchini.
Simbachawene alisema suala hilo
limeshughulikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura),
Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).
“Kwa hali ya sasa tatizo hili
limeshughulikiwa tumeamua kuchukua mafuta ya on transit (yanayopitia
nchini kwenda nje ya nchi),” alisema.
Alisema kwa upande wa Dar es Salaam tatizo
hilo limekwisha kwa kuwa mafuta yameshajaa na magari makubwa yameanza
kuchukua mafuta kwenda mikoani.
“Tunaamini kuwa tatizo hili halitarejea
tena,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa waziri atatoa taarifa rasmi
kwa kuzungumza na waandishi wa habari.
Akifunga hoja hiyo, Spika aliagiza serikali itoea taarifa rasmi siku ya Jumatatu bungeni.
EWURA YATOA TAARIFA TOFAUTI
Kwa upande wake Ewura imesema katika
kukabiliana na uhaba wa mafuta, serikali imezuia lita milioni 40 za
mafuta zilizokuwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi. Mafuta hayo sasa
yanatarajiwa kuuzwa nchini ili kuziba pengo linalotokana na uhaba
uliopo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema
akiba ya lita milioni 80 zilizokusudiwa kusafirishwa kwenda nje,
zilipunguzwa kwa kiwango cha asilimia 50.
Alisema serikali imeshatoa vibali kwa
baadhi ya kampuni za mafuta, ili ziyauza hapa nchini ambapo mpaka sasa,
kampuni tisa zimeridhia maombi hayo. Hatua hiyo itawezesha `kusambaza’
lita milioni 26.6 za petroli na diseli pamoja na mafuta ya taa yenye
ujazo wa lita milioni 1.48.
Hata hivyo, wakati Simbachawene akisema
mafuta hayo yameshasambazwa sokoni, Kaguo alisema utekelezaji wake
haujaanza, kwa vile kampuni hizo hazijatimiza masharti ya Mamlaka ya
Mapato (TRA) ikiwemo kulipa kodi ya asilimia 100.
Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Mogas,
Gapco, GBP, Lake Oil, Hass Petroleum, Puma, Oryxy, Engen na Camel. Hata
hivyo, alisema tatizo la mafuta linatarajiwa kumalizika kwa kipindi
kifupi (hakutaja) ambapo meli zilizoshindwa kupakua mafuta kutokana na
kukosa nafasi ya kutia nanga, zitakakapofanya hivyo.
Alisema kutokana na ucheleweshaji, meli
hizo zilisubiri kwa siku 19 bila kupakuliwa, hivyo kutumika kwa akiba ya
Agosti mwaka huu, iliyokuwa kwa wafanyabiashara. Kwa mujibu wa Kaguo,
kipindi hicho hapakuwa na meli iliyoleta mafuta, hivyo kusababisha uhaba
wa mafuta bidhaa hiyo.
Hata hivyo, Kaguo alisema kuanzia Novemba 6 hadi 9 mwaka huu, meli zitaanza kupakuliwa mafuta na kuanza kuingia sokoni.
Akizungumzia akiba ya mafuta yaliyopo kwa
sasa alisema kuwa kuna diseli lita milioni 35.8 ambayo ni matumizi ya
siku 10, petrol lita milioni 16.2 ambayo ni matumizi ya siku tisa. Pia
alisema yapo mafuta ya ndege yapo lita milioni 11.7 matumizi ya siku 25
na mafuta ya taa yapo lita 558,180.
WAZIRI AJITOKEZA , ATANGAZA KUFUTA LESENI ZA MAFUTA
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, alisema uamuzi alioufikiwa ulitokana na kampuni za
mafuta kufanya kazi kinyume cha taratibu huku wajumbe wa PIC wakihusika
kulinda maslahi yao kibiashara.
Uamuzi huo, aliutangaza jijini Dar es Salaam jana jioni, baada ya kukutana na wafanyabiashara ya mafuta na waandishi wa habari.
Alisema sababu ya uhaba wa mafuta ni kile
alichokiita kuwa ni ‘mvutano wa kizembe’ kati ya Ewura, bodi ya PIC na
wafanyabiashara.
Profesa Muhongo alisema kutokana na
mvutano huo, baadhi ya wafanyabiashara waliamua kupeleka mafuta nje ya
nchi, wengine wakayaficha kwenye maghala kwa kisingizio kuwa bei elekezi
haiwalipi faida.
Alisema kuna baadhi ya kampuni zilipewa
leseni ya kuagiza mafuta, lakini biashara zao zilikuwa za mfukoni na
kuisababishia serikali hasara na usumbufu.
Kutokana na hali hiyo, aliiagiza Ewura
kuzifutia leseni kampuni zilizoshindwa kuingiza mafuta kwa kipindi cha
miezi sita na taarifa hiyo kumfikia Jumatatu ijayo.
Profesa Muhogo alisema bodi ya PIC
imevunjwa kutokana na kuwa na wafanyabiashara ambao kazi kubwa
walioifanya ni kulinda biashara zao.
“Sasa bodi mpya itakayoundwa itakuwa ya
kisasa na itakuwa na mjumbe mmoja mmoja kutoka idara husika na
mwenyekiti atatoka wizarani,” alisema.
Alisema wajumbe wa bodi hiyo wataoka
Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari (TPA), Kampuni ya kupakua na
kupakia makontena bandarini (TICTS), PIC na Ewura.
Alisema bodi mpya inatarajiwa kuanza kazi ifikapo Jumanne ya wiki ijayo.
MNYIKA: POKEENI TAARIFA ZA SERIKALI KWA TAHADHARI
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John
Mnyika, amesema umma unapaswa kupokea kwa tahadhari taarifa zinazotolewa
na Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake nje ya Bunge.
Alisema taarifa hizo ni zile zinazohusu
masuala ya sekta ya nishati ikiwemo uhaba wa mafuta uliopo sasa, hivyo
kusisitiza umuhimu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter
Muhongo, atoe taarifa bungeni kuhusu masuala tajwa.
Aidha, Mnyika alisema Spika Makinda
anapaswa kutoa maelezo bungeni ya kuelekeza Kamati ya Kudumu ya Bunge,
itakayochambua ukweli wa taarifa hizo.
“Kujirudia mara kwa mara matatizo katika
sekta za nishati hususan katika biashara ya mafuta, kumechangiwa na
sababu za udhaifu wa kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji wa
baadhi ya viongozi na watendaji wengine…” alisema Mnyika.
Mnyika alidai kuwepo taarifa kuwa uhaba
huo ni matokeo ya baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta, kuficha
petroli na dizeli wakisubiri kutangazwa kwa bei mpya ya bidhaa hizo.
Kwa mujibu wa Mnyika, matatizo katika
biashara ya mafuta hayahusu uhaba wa dizeli na petrol tu, bali pia
kasoro katika ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
No comments:
Post a Comment