Serikali imeombwa kumwondoa Mkurugenzi
wa Fedha na Utawala wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Mbonimpaye Mpango kwa
madai kwamba anawashawishi wanafunzi kumkataa Mkuu wa Chuo hicho, Abuu
Mvungi.
Ombi hilo lilitangazwa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho,
Frank Nkinda, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini
Dar es Salaam.
Alisema kumekuwa hakuna maelewano mazuri kati ya Mkurugezi na Mkuu wa chuo kitendo ambacho kinawaumiza wanafunzi.
“Sisi Wanafunzi tunatamka Mpango maarufu kama mama mpango kuondoka
chuoni hapa kwa kuwa amekuwa mwiba na chanzo cha migogoro,” alisema
Nkinda.
Alisema Mpango amekuwa akikwamisha shughuli za wanafunzi kwa kupandisha
ada kiholela kwa lengo la kuifanya Taasisi ikose wanafunzi ili utendaji
wa Mkuu wa taasisi uonekane mbovu.
Nkinda alisema kutokana na hila hizo Mkurugenzi huyo amekuwa akipeleka
taarifa za uongo serikalini kuwa wanafunzi hawamtaki mkuu, kumbe yeye
ndiye mwenye matatizo ya kutoelewana naye.
NIPASHE ilimtafuta Mkurugezi wa Chuo hicho kwa njia ya simu ili kujua
juu ya tuhuma hizo, simu haikupokelewa wala ujumbe mfupi wa maandishi
haukujibiwa.
NIPASHE ilipomtafuta Mkuu wa Chuo hicho simu zake zote za mkononi hazikupatikana.
No comments:
Post a Comment