TASNIA ya filamu nchini imeendelea kukumbwa na simanzi baada ya
wasanii wawili, Halid Mohamed maarufu kama 'Mlopelo' na John Maganga
kufariki dunia wiki hii.Baada ya Mlopelo kuzikwa juzi, habari nyingine
zilizopatikana jana ni kufariki kwa msanii Maganga katika hospitali ya
Muhimbili juzi.
Rais wa Shirikisho la Sanaa Tanzania, Jacob Steven JB alithibitisha kutokea vifo hivyo na kusema wamepoteza watu muhimu kwenye sanaa ya filamu.
"Tunasikitika kutokea kwa vifo vya wasanii wenzetu. Walikuwa na mchango mkubwa katika kuisukuma sanaa hii kwenda hatua ya mafanikio," alisema JB.
"Wasanii wote tupo kwenye maombolezo makubwa na tunawapa wafiwa wote pole kutokana na misiba hii," alisema zaidi JB.
JB aliongeza kuwa taarifa kuhusu ratiba ya Maganga zitatolewa na uongozi wao wa juu.
Taarifa za awali zinadai kuwa Maganga alifariki baada ya kuumwa tumbo na kuwahishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kufariki usiku wa kuamkia jana.
No comments:
Post a Comment