HABARI MOTO MOTO ...
Tuesday, November 27, 2012
Yanga kwenda Uturuki Des. 27
Uongozi wa klabu ya Yanga umesema timu yao itaondoka nchini Desemba 27 mwaka huu kuelekea Uturuki ambako itaweka kambi yake kujifua kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano ya klabu hiyo, Abdallah Bin Kleb aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kocha wa timu hiyo, Mholanzi Ernie Brandts kutoa pendekezo hilo.
Alisema kuwa kamati yake baada ya kukaa na kujadiliana na kocha huyo, imeamua timu ikaweke kambi ya mafunzo nchini humo kwa kipindi cha wiki mbili na kwamba kocha amewaambia nchi hiyo hutoa huduma bora za kambi za michezo.
“Timu yetu imeanza mazoezi rasmi leo (jana) asubuhi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na mashindano ya Kombe la Kagame yatakayoanza mwezi Januari mwakani,” alisema Bin Kleb.
“Hii itatoa fursa kwa wachezaji wote kujumuika pamoja kwani kwa sasa baadhi ya wachezaji wetu wapo wanazitumikia timu zao za taifa kwenye mashindano ya Chalenji nchini Uganda.
“Hivyo mara tu mashindano ya Chalenji yatakapomalizika, watarejea nchini kujiunga na mazoezi na wachezaji wenzao tayari kujiandaa na safari hiyo… kocha ana uzoefu na nchi ya Uturuki, hivyo kwa mapendekezo yake, tulimkubalia na kuanza kuandaa maandalizi ya kambi hiyo lengo ikiwa ni kuifanya timu yetu icheze soka safi la burudani na ushindi.”
Mwenyekiti huyo ambaye pia alifanikisha usajili wa Mrwanda mwenye asili ya Kongo, Mbuyu Twite, alisema kuwa wakiwa Uturuki, watacheza mechi mbili za kirafiki na timu za nchi hiyo ambazo hata hivyo hakuzitaja.
Aidha, Bin Kleb alisema kuwa wamepokea mapendekezo ya kocha wao kuhusu wachezaji wanaopaswa kubaki, kuondolewa na kusajiliwa wakati wa ‘dirisha dogo’ la usajili litakalofungwa Desemba 25 mwaka huu na watalitolea ufafanuzi baadaye suala hilo.
“Hatupendi masuala ya kukurupuka kutangaza vitu ambavyo havijakamilika, ndiyo maana hata usajili wetu uliopita tulitangaza baada ya kukamilisha kila kitu,” alisema.
Kuhusu kutakiwa na klabu za nje kwa wachezaji wao wawili, kiungo Mrwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na mshambuliaji Didier Kavumbagu raia wa Burundi, Bin Kleb alisema bado wanafanya mazungumzo na klabu hizo.
Fabregas anatakiwana klabu ya El Merreikh ya Sudan wakati Kavumbagu anayeongoza kwa magoli msimu huu, ametengewa dola za Marekani 10,000 na klabu moja ya Qatar ili aondoke Jangwani.
Katika hatua nyingine, Bin kleb alisema kuwa klabu hiyo itamtangaza afisa habari mpya wa klabu hiyo atakayerithi mikoba ya Louis Sendeu kabla ya Desemba 15 mwaka huu.
“Tunatambua umuhimu wa kuwa na afisa habari wa klabu yetu. Tutamtangaza kabla ya Desemba 15 na ripoti kamili kuhusu masuala mbalimbali ya Yanga tuitoa Desemba 8 mwaka huu wakati wa Mkutano Mkuu na wanachama wa klabu hii,” alifafanua zaidi Bin Kleb.
Licha ya kuanza ligi vibaya kwa vipigo viwili na sare moja katika mechi nne za kwanza hadi kufikia kumfukuza kocha aliyewapa ubingwa wa klabu bingwa Afrika Mashariki (Kombe la Kagame), Mbelgiji Tom Saintfiet, waliyedumu naye kwa siku 80 tu, Yanga walimaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni kwa pointi 29 wakifuatiwa na Azam (24) na Simba (23).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment