*Vyama vyahaha kuelezea usafi wa hesabu zao kabla ya kunyimwa ruzuku
KAULI ya Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaka kusitishwa utoaji
ruzuku kwa vyama vya siasa hadi pale hesabu zao zitakapokaguliwa,
inaonekana kuwachanganya viongozi wa vyama hivyo.
Zitto alisema jijini Dar es Salaam
juzi kwamba jumla ya Shilingi bilioni 67.7 zimetolewa na Serikali na
kupewa vyama tisa vya siasa, lakini hadi sasa hesabu zao hazijakaguliwa
na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Jana, Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kiliibuka na kusema hesabu zao ziko makini, kwani zimekaguliwa na
wakaguzi wa hesabu wa nje kwa maelekezo ya CAG.
Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema CCM imekuwa ikitekeleza utaratibu
wa kukaguliwa hesabu zake tangu mwaka wa fedha 1977/78 kilipoanzishwa
hadi 2003/4, ambapo hesabu zao zilikuwa zikikaguliwa na Tanzania Audit
Corporation (TAC).
Alisema hesabu za chama hicho
kikongwe cha siasa barani Afrika ziliendelea kukaguliwa na Januari 29
mwaka huu, CCM ilimwomba CAG awapangie mkaguzi wa hesabu za 2011/2012,
CAG akawapangie kampuni ya TAC-Associates, kampuni itakayoendelea
kukagua hesabu za CCM hadi 2013/2014.
“Hesabu zilizokaguliwa zote zipo kwa
CAG na za 2011/2012 ziko mikononi mwa TAC-Associates, wakimaliza
zitawasilishwa kwenye vikao vya chama na baadaye kwa CAG,” alisema
Nape.
Nape aliitetea CCM dhidi ya kauli ya Zitto ya kuzuia kupewa ruzuku na kwamba wapo tayari kukutana na PAC.
“Huenda kauli ya Zitto imekilenga
chama chake mwenyewe kinachodaiwa kufanya matumizi mabaya ya fedha za
ruzuku kwa viongozi wake kukopeshana bila kufuata utaratibu,” alisema.
Zitto ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza na RAI kuhusu kukaguliwa
kwa hesabu za CCM, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alionyesha kushangazwa
na kauli za Nape kuhusu hesabu za chama hicho tawala.
Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini
mwenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Chadema alisema kuwa CAG hana
hesabu za CCM, na kusisitiza kuwa hakuna chama chochote kitakachopata
ruzuku hadi baada ya kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu za kipindi
cha miaka minne.
“Kama CCM wanasema wamefanyiwa
ukaguzi, basi hesabu zao zimekaguliwa na mkaguzi wa kichochoroni. CAG
hazijui, hana taarifa za hesabu za CCM kwa kipindi cha miaka minne
iliyopita.
“Hayo ni makosa, na si wao tu, bali
vyama vyote vinavyochukua fedha za walipa kodi wa Tanzania na kuzitumia
hovyo, havitapata tena ruzuku hizo,” alisema.
Awali, Zitto alitoa agizo hilo baada
ya kamati yake kumaliza mkutano wake na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi jijini Dar es Salaam, akisema hesabu hizo ni za kuanzia
mwaka wa fedha wa 2009/10.
Vyama hivyo ni CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, TLP, APPT Maendeleo na Chausta.
Jana Nape alimshambulia moja kwa moja
Zitto kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, akitaka awajibike kutokana na
kile alichodai kuwa ni ufujaji mkubwa wa fedha ndani ya Chadema, chama
kikuu cha upinzani.
“Sote tunafahamu kuhusu kelele
zilizopo mtaani juu ya matumizi mabaya ya ruzuku Chadema. Wanachama kule
wanalalamika sana na kuwalaumu viongozi wao. Si ajabu hawa jamaa wakawa
wanakiuka sheria hii. Zitto awashughulikie wao kwanza,” alisema Nape.
Zitto hakushitushwa na kauli hiyo ya
Nape na aliliambia RAI kwamba, anachokifanya ni kutimiza wajibu wake
kama Mwenyekeiti wa PAC na wala si kumkonoa yeyote ndani au nje ya
Chadema.
“Vyama vyote vitakaguliwa ikiwa ni
pamoja na Chadema. Ukweli utajulikana na kama kuna hatua zitachukuliwa.
Si kukomoana,” alisisitiza Zitto.
Hata hivyo, RAI lilidokezwa na
mwanachama mmoja wa Chadema kwamba kumekuwapo na mitafaruku ya chini kwa
chini ndani ya Chadema kuhusu matumizi ya fedha, iwe za ruzuku au
misaada kutoka kwa wafadhili.
Chanzo cha uhakika kutoka Makao Makuu
ya Chadema, Mtaa wa Mfipa, Kinondoni ambacho ni wazi hatuwezi kukianika
hadharani, kilisema kuna fedha nyingi zilizotolewa kwa ajili ya
mikutano ya Vuguvugu la Mabadililo (M4C) lakini hazikutumika kama
ilivyokusudiwa.
Mtoa taarifa wetu alidai kuwa posho
na marupurupu ya viongozi kadhaa na wake zao ni za kutisha na kutia
shaka hesabu za chama hicho hata kabla PAC haijataka kukaguliwa kwake.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Julius Mtatiro akizungumzia suala hilo la
ukaguzi wa hesabu alisema huenda Katibu wa Bunge haijapewa taarifa
sahihi kuhusu chama hicho, akidai kuwa kiliandikiwa barua ya kutakiwa
kufanyiwa ukaguzi kwa sharti la kumlipa CAG.
“Ilikuwa mwaka 2011 CAG alipotuarifu
kuwa kuna taasisi imeteuliwa kwa ajili ya kufanya ukaguzi, tukauliza
inakuwaje kazi inayofanyika ni ya Serikali sisi tumlipe mkaguzi?
“Hofu yetu ilikuwa kwamba tungeweza
kutuhumiwa kumuhonga mkaguzi huyo. Sasa huenda Zitto hajapewa taarifa
sahihi kabisa,” alisema Mtatiro.
Kwa mujibu wa sheria, CAG analo fungu lake kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kamwe hapaswi kulipwa na mteja anayekaguliwa.
Wadadisi wa mambo wanasubiri kwa hamu
kuona ninikitatokea ndani ya vyama hivyo vikubwa vya siasa nchini; CCM,
Chadema na CUF kama vikishindwa kuhalalisha matumizi ya fedha za ruzuku
walizopewa.
.jpg)
No comments:
Post a Comment