HABARI MOTO MOTO ...

Monday, October 21, 2013

`Uncle J` hatunaye

Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Radio One, Julius Nyaisanga (53), maarufu kama ‘Uncle J’ amefariki dunia. Nyaisanga alifariki jana asubuhi katika Hospitali ya Mazimbu, mjini Morogoro baada ya kuugua ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu matatizo yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu. Mtangazaji huyo maarufu na mkongwe nchini mauti yamemkuta akiwa Meneja Mkuu wa Abood Media. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Matangazo wa Abood Media, Abed Dogoli, alisema alipokea taarifa ya kifo cha Nyaisanga jana asubuhi na kusema alifariki dunia jana hiyo majira ya saa 1:00 asubuhi katika Hospitali ya Mazimbu, iliyopo Manispaa ya Morogoro. Alisema taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu eneo la Kihonda, mjini hapa. Alisema wanatarajia kumsafirisha kwenda nyumbani kwao mkoani Mara kwa maziko na kwamba, taarifa zaidi zitatolewa kama kutakuwa na mabadiliko. Hata hivyo hakusema mazishi hayo yatafanyika lini. Kwa upande wake, Mke wa marehemu, Leah Nyaisanga, alisema enzi ya uhai wake, mumewe aliwahi kufanya kazi Radio Tanzania (RTD), pia aliwahi kufanyakazi IPP Media akiwa kama mtangazaji Radio One na baadae alipandishwa cheo hadi kuwa Mkurugenzi wa radio hiyo. Alisema marehemu pia aliwahi kufanya kazi Radio Deutsche Welle ( DW) ya nchini Ujerumani. Kwa mujibu wa Leah, mumewe pia aliwahi kwenda katika nchi za Marekani, Japan na Ghana kwa kazi za habari. .Alisema juzi jioni, hali ya mumewe ilibadilika ghafla na kuzidiwa na kukimbizwa Hospitali ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro, na kwamba, alifikwa na umauti jana asubuhi. Marehemu Nyaisanga ameacha mke mmoja na watoto watatu, ambao ni Samuel, Noela na Beatrice. Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Aziz Abood, ambaye familia yake ndiyo wamiliki wa Kituo cha Abood Media alisema amepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Nyaisanga akimwelezea kuwa alikuwa mchapakazi hodari. Alisema alimfahamu Nyaisanga miaka mingi tangu akiwa katika vituo mbalimbali vya utangazaji na alikuwa mahiri katika utangazaji na maarufu. Kabla ya kwenda Aboud Media, Nyaisanga alikuwa Mkurugenzi wa Radio One akiwa ni mmoja wa watangazaji waanzilishi wa radio hiyo akitokea Radio Tanzania (RTD). Nyaisanga atakumbukwa kwa sauti yake nzuri na utangazaji wake mahiri, ucheshi na kupenda kushirikiana na watu wengine.

No comments:

Post a Comment