Wanachama hao ambao ni kikundi cha Mbezi A na B wamedai kuwa mpaka
sasa imeshapita miaka mitatu wamekuwa wakipigwa kalenda kila wakati kuwa
watapatiwa akiba zao jambo ambalo limeshindikana kutekelezeka.
Malalamiko hayo ambayo yametolewa na Mwenyekiti wa kikundi cha
Mbezi A, Mahija Yusuph, alisema kuwa wanashindwa kuelewa ni kwa nini
mfuko huo unawacheleweshea kuwapa akiba zao wakati tayari wameshamaliza
kulipa mkopo.
Alisema kuwa tangu mwaka 2010 walitakiwa kupatiwa akiba zao na
matokeo yake kila wakati wanaambiwa wasubirie bajeti ipitishwe na
ikishapita, hawapatiwi fedha zao.
Yusuph alisema kuwa kuna wengine walijaza fomu za kupatiwa mkopo
lakini mpaka sasa hawajapatiwa. “Sisi tuliwauliza akiba zetu mmekaa nazo
kwa muda mrefu vipi mtatulipa na riba lakini wametukatalia na kusema
kuna baadhi hawakumaliza mkopo tukawajulisha watukate hilo deni la
wenzetu na kiasi kilichobakia watulipe fedha zetu lakini tunapigwa
kalenda,” alisema.
Alisema kuwa kabla ya kulazwa hospitali kwa mwezi alifuatilia fedha
hizo na kujulishwa zitatolewa Januari mwaka huu kuanzia tarehe 2 jambo
ambalo halikufanyika.
Alisema aliporuhusiwa kutoka hospitali alifuatili fedha hizo na
kujulishwa kuwa wasubirie wiki mbili.
Yusuph alisema idadi ya watu waliokuwapo kwenye kikundi hicho
walikuwa 40 na kwa sasa wamepungua nakufikia 20 kwa kuwa wameona hawana
imani na mfuko huo.
Naye Katibu wa kikundi hicho, Rehema Marima, alisema kuwa mfuko huo
huenda ukawa umekufa lakini hawapo wazi.
Alisema baada ya kumaliza mikopo yao wengine walijaza fomu za mkopo
lakini mpaka sasa miaka mitatu imepita hawajajulishwa jambo lolote.
Marima alisema wao wanachokitaka ni kupatiwa akiba zao kwani
wamechoka kupigwa kalenda kila wakati na kupoteza muda wao kufuatilia.
Alisema kuwa siyo kikundi chao tu kinachodai wapo wanachama wengi
wanaodai na hawajui hatima yao ni nini.
Hata hivyo, alisema na kikundi cha Mbezi B kinawadai akiba zao na
wenyewe hawajui nini hatima ya fedha zao.
NIPASHE ilizungumza na Mkurugenzi wa PTF, Haigath Kitala, ambaye
alieleza kuwa mfuko wake unatambua akiba zinazodaiwa na wanachama wake
na kwamba watakapopata watazitoa kwa wakati.
Alisema kuwa mfuko upo hai na wanatambua madeni ya wanachama wake
kwani wana kumbukumbu ya kila mwanachama.
Kitala alisema taarifa aliyonayo ni kwamba kituo cha Mbezi A,
wanadai akiba zao za Sh. milioni 8.17 na wenyewe wanadaiwa mkopo wa Sh.
milioni 4.25 ambazo wanachama wake hawakuzirejesha kama wanavyotakiwa.
Alisema kwa upande wa kituo cha Mbezi B, wanadai akiba ya Sh.
8,963,400 na mfuko huo unawadai Sh. 7,526,400.
Kitala alisema kwa wale ambao wanadai akiba zao wanatakiwa kufika
ofisini kwao kwa ajili ya kupatiwa taarifa na siyo kusikiliza
wasiohusika.
Alisema kwa sasa mfuko unasubiri kupatiwa fedha ili waanze kulipa
madeni hayo kwani kuna matawi mengine ambayo yanadai fedha.
Madhumuni ya Mfuko wa PTF ni kuwasaidia wananchi wa kipato cha
chini kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu ili waweze kujikwamua
kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment