MKALI wa muziki wa hip hop nchini, Emmanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’ amesema mlinzi wake ni Mungu na hana muda wa kutafuta wa kumlinda au kuhangaika kwa waganga wa kienyeji.
Kauli hiyo imekuja baada ya kusemekana kwamba, kuna wasanii ambao walisafiri kwenda mkoani Tanga kwa ajili ya kumroga msanii huyo ili apunguze kasi ya kuimba na kuacha kuwataja watu mbalimbali katika nyimbo zake.
Akizungumza katika mahojiano na Clouds FM, Ney alisema, alipigiwa simu na mganga huyo na kuelezwa kwamba, kuna watu ambao walifika kwake na kumtaka yeye amtumie radi au amfanye apoze viungo vya mwili kutokana na kuwaimba katika baadhi ya nyimbo zake.
“Kwa maana hiyo, hao watu walitaka kuniua, lakini nilipomuuliza mganga huyo kwamba ni kina nani, alisema hawezi kuniambia moja kwa moja mpaka atakapopata ruhusa ya kunitajia kutoka kwa mizimu yake kama alivyopewa ruhusa ya kuniambia,” alisema Ney na kuongeza:
“Mimi siogopi lolote, sina haja ya kutafuta ‘bodigadi’ wala askari wa kunilinda, mlinzi wangu ni Mungu na najiamini sina haja ya kuogopa lolote, hao watu wanajisumbua tu, kama wao ni wasanii kwanini wasifanye kazi nzuri kila mmoja azione?”
Nyimbo ambazo Ney wa Mitego ametaja baadhi ya majina ya watu ndani yake ni ‘Salamu Zao’ na ‘Nasema Nao’.


No comments:
Post a Comment