Na Joachim Mushi, Thehabari.com
USAFIRI wa kutumia treni jijini Dar es Salaam kutokea eneo la Ubungo
Maziwa kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Stesheni ya Treni)
umeanza leo. Treni ya kwanza imeondoka Ubungo majira ya saa 12:00
asubuhi kuelekea katikati ya jiji, ambapo kwa mujibu wa maofisa wa
Shirika la Reli Tanzania (TRC) imetumia wastani wa dakika 30 kufika
katikati ya jiji.
Treni ilioanza kazi leo iliyokuwa na injini mbili (vichwa vya traini)
moja ikiwa imefungwa nyuma na nyingine mbele huku ikiwa na mabehewa
sita, yaani matano ya abiria wa kawaida (watu wazima) na moja likiwa ni
maalumu kwa ajili ya kubeba wanafunzi. Abiria mmoja ni sh. 400 kwa tripu
huku wanafunzi wakitakiwa kulipa sh. 100 kwa kila mmoja.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ndiye aliyezindua usafiri
wa leo ambao ni wamajaribio, akiwa pamoja na viongozi waandamizi kutoka
TRC, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja
na Polisi Kitengo cha Reli. Treni hiyo pia imezinduliwa pamoja na treni
ya TAZARA ambayo itafanya kazi kama ya Ubungo, lakini yenyewe ikianzia
eneo la TAZARA kuelekea Mwakanga.
Akizungumza mara baada ya ufunguzi huo Waziri Mwakyembe alisema
atahakikisha treni hiyo inaendelea kufanya kazi ili kuwasaidia kiusafiri
wananchi wa Dar es Salaam ambao wamekuwa wakisumbuliwa na kero ya
usafiri hasa kwa foleni, ambapo utumia muda mrefu njiani kuingia na
kutoka jijini.
Alisema jumla ya mabehewa ya treni 14 pamoja na injini mbili
zimekarabatiwa na mafundi wazalendo nchini, ambayo ndiyo yatakayokuwa
yakifanya kazi ya kusafirisha abiria kuingia na kutoka jijini kila
asubuhi na jioni. Alisema kwa sasa inafanya treni moja kwa majaribio
lakini baada ya uzinduzi mkubwa zitafanya kazi treni mbili, na zitakuwa
zikipishana njiani moja ikirudi na nyingine ikienda.
Akifafanua zaidi alisema kitendo cha mafundi wazalendo kufanya
ukarabati kwa mabehewa na injini kimeokoa kiasi kikubwa cha fedha za
umma kwani ukarabati wote umetumia sh. bilioni 2.1 tu, ilhali kama
Serikali ingelazimika kukodi injini gharama ingekuwa kubwa zaidi kwani
bei ya kukodi injini moja ya treni ni sh. milioni moja kwa siku.
Hata hivyoDk. Mwakyembe amewataka Watanzania hasa abiria kuwa
wavumilivu kwa upungufu utakaojitokeza kwa safari za mwanzo kwani bado
wanaendelea kufanya marekebisho kadhaa, lakini baada ya muda mambo
yatakaa sawa. Mwandishi wa habari hizi alikuwa ni mmoja wa wasafiri
walioizindua treni hiyo leo.
Awali akizungumza mmoja wa viongozi waandamizi wa TRC, alisema treni
hiyo itafanya kazi kila siku isipokuwa kwa siku za jumapili na siku kuu
na itaanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa sita mchana na kupumzika hadi saa
9:00 za jioni, itakapoendelea tena na safari zake hadi majira ya saa
nne usiku.
Uchunguzi uliofanywa na muandishi wa habari hizi umebaini kuwa behewa
moja la treni linauwezo wa kuchukua abiria 66 wakiwa wamekaa, lina
milango minne, feni, taa, muziki/redio, pamoja na mikanda maalumu ya
kujishikia kwa abiria ambao watakuwa wamesimama.
Aidha mabehewa yote yana madirisha ya kutosha kuingiza na kutoa hewa
ya kutosha. Treni ilioanza kazi leo, ikitokea Ubungo ilikuwa ikisimama
vituo vya eneo la Mwananchi (relini), Tabata Relini, Buguruni Miamani,
Tazara, Kariakoo Gerezani (Kamata), na mwisho Kituo Kikuu cha Treni
kilichopo jirani na Kituo cha Polisi Kati (Katikati ya Jiji)
No comments:
Post a Comment